Umma wa Ukraine wakabidhiwa tuzo ya uhuru ya Umoja wa Ulaya
14 Desemba 2022Tuzo hiyo ya Sakharov ya uhuru wa mawazo na fikra imetolewa siku ya Jumatano kwa umma wa Ukraine kuenzi mapambano ya raia wa taifa hilo dhidi ya uvamizi wa Urusi.
“Hakuna mwingine anayestahili tuzo hii” amesema rais wa Bunge la Ulaya Roberta Metsola katika halfa ya kutunuku tuzo hiyo iliyohudhuriwa na wawakilishi wa raia wa Ukraine walioipokea tuzo kwa niaba yaw engine.
“Kwa Waukraine wote waliopoteza ndugu na marafiki. Kwa wote waliosimama na kupigania kile wanachokiamini“. Amesema Metsola katika sehemu ya hotuba aliyoitoa.
Tuzo hiyo, iliyopewa jina lake kwa heshima ya mkosoaji mkubwa wa iliyokuwa Dola ya Kisovieti, Andrei Sakharov, imekuwa ikitolewa kila mwaka tangu mwaka 1988 kwa watu na mashirika yanayolinda haki za binadamu na misingi ya uhuru. kwa watu na mashirika yanayolinda haki za binadamu na misingi ya uhuru.
Washindi wa zamani ni pamoja na Alexei Navalny
Mwaka uliopita tuzo hiyo ilitolewa kwa mpinzani mkubwa wa ikulu ya Kremlin, Alexei Navalny kwa juhudi zake za kumtunishia msuli rais Vladimir Putin wa Urusi kutokana na utawala wake wa mabavu. Mshindi wa mwaka huu alitangazwa mwezi Oktoba.
Umma wa Ukraine uliwakilishwa na mfanyakazi wa kijitolea wa huduma za dharura kutoka shirika liitwalo Taira´s Angels, Yulia Pajevska, mwanasheria wa haki za biandamu Oleksandra Matviychuk na meya aliyefukuzwa kutoka mji uliokamatwa na Urusi wa Melitopol, Ivan Fedorov.
“Ni ishara isiyo mfano kuwa mwaka huu umma wa Ukraine unapokea tuzo ya Sakharov kwa sababu raia wana nafasi muhimu kuliko wanavyofikiria”, amesema Matviychuk, ambaye pamoja na Fedorov, wameomba nyongeza wa msaada wa silaha kwa Ukraine.
“Tunahitaji vitu kadhaa, tunahitaji silaha, vikwazo na haki pamoja na msaada wa kuijenga upya nchi yetu” wamesema wawili hao.
Tuzo hiyo huambatana na zawadi ya kitita cha dola 53,000 ambazo zitagawanywa kwa wawakilishi wa asasi za kiraia nchini Ukraine.
Urusi ambayo inaitaja vita nchini Ukraine kuwa operesheni yake maalum ya kijeshi, inadhibiti maeneo makubwa ya kusini na mashariki mwa nchi hiyo licha ya kupata pigo kwenye miji kadhaa ambayo vikosi vyake vimekuwa wakiishikilia tangu nchi hiyo ilipotuma jeshi lake nchini Ukraine mnamo mwezi Februari.