1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Umoja wa Mataifa wataka kupelekwa kikosi cha amani Sudan

Saleh Mwanamilongo
6 Septemba 2024

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamelaumu pande zote mbili zinazozona nchini humo kwa uhalifu wa kivita ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na mateso.

Mohamed Chande Othman (kulia ), Steven Ratner na Radhika Coomaraswamy - Wajumbe wa Tume ya Kimataifa ya Wataalamu wa Haki za Binadamu kuhusu Sudan
Mohamed Chande Othman (kulia ), Steven Ratner na Radhika Coomaraswamy - Wajumbe wa Tume ya Kimataifa ya Wataalamu wa Haki za Binadamu kuhusu SudanPicha: Todd Pitman/OHCHR

Ujumbe wa wataalamu hao ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa umesema leo kwamba pande zinazopigana vita nchini Sudan zimewanyanyasa raia kwa kiwango cha juu, kinachoweza kufananishwa na uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Mwenyekiti wa ujumbe huo, Mohammed Chande Othman, amesema alipowasilisha ripoti yao ya Fact Finding yenye kurasa 19 kwamba jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF waliwashambulia raia, kuwatesa na kuwakamata kiholela.

"Watu wa Sudan wameteseka sana, na ukiukwaji dhidi yao lazima ukome. Hili haliwezi kufanywa bila kumaliza mapigano na kwa hivyo juhudi zote lazima ziwekezwe katika kufikia usitishaji vita.", alisema Chande Othman.

Kupelekwe kikosi cha kulinda amani

Uchunguzi wao ulihusisha mahojiano na wahanga 182, ndugu na mashuhuda na kupendekeza kuwekwa vizuizi vya silaha na kupelekwa kwa kikosi cha kuwalinda raia. Wataalam hao walitoa wito wa kuongezwa kwa vikwazo vya silaha katika nchi nzima mbali na jimbo la Darfur hivi sasa.

"Kutokana na kushindwa kwa pande hasimu kulinda raia hadi sasa, ni muhimu kupelekwa kikosi huru na chenye nguvu na mamlaka ya kuwalinda raia nchini Sudan.", imesema ripoti ya wachunguzi.

Hata hivyo wataalam hao hawakueleza vipi kikosi hicho kinaweza kuundwa, na wala hawakutaja nchi ambazo zinaweza kuhusika katika uhalifu wa Sudan kwa kuunga mkono pande hasimu.

Serikali ya Sudan ilikataa kutoa maoni rasmi kuhusu ripoti ya matokeo ya ujumbe huo wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Hali mbaya ya kibinadamu

Mashirika ya misaada yametoa tahadhari leo Jumanne kwamba Sudan inakabiliwa na baa la njaa ambalo halijawahi kutokea katika historiaPicha: Mohamed Khidir/Xinhua/picture alliance

Machafuko hayo ya Sudan yamesababisha mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani. Makumi ya maelfu ya watu wameuawa, na wataalamu hao wamesema raia milioni nane wameyakimbia makazi yao huku wengine milioni mbili wakikimbilia nchi jirani.

Mzozo huo wa Sudan, unaoendelea kwa miezi 17 sasa, unahusisha jeshi la taifa linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan dhidi ya wanamgambo wa RSF wa naibu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Daglo. Vita vilivyoanza mjini Khartoum mwezi Aprili mwaka jana vimeenea hadi majimbo 14 kati ya 18 ya nchi hiyo.

Juhudi za kidiploamisia

Mwezi Agosti, Marekani iliitisha mazungumzo mjini Geneva yenye lengo la kumaliza vita huko Sudan. Mazungumzo hayo yaliafiki upatikanaji wa misaada, lakini pasina kufikia hatua ya usitishaji mapigano.

Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Umoja wa Afrika na Umoja Mataifa pia zilihusishwa katika mazungumzo hayo.

Marekani pia ilitangaza vikwazo vya viza kwa idadi isiyojulikana ya watu binafsi nchini Sudan Kusini, ikiwa ni pamoja na maafisa wa serikali, wanaotuhumiwa kuzuia utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa Wasudan milioni 25 wanaokabiliwa na njaa kali.