1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika kukomesha ndoa za utotoni

26 Novemba 2015

Umoja wa Afrika unakutana katika mji mkuu wa Zambia, Lusaka, katika mkutano wenye lengo la kujadili njia za kujaribu kukomesha tamaduni na mila zinazohalalisha ndoa watoto.

Nigeria Proteste gegen Kinderehe
Picha: picture alliance/AP Photo

Kwa mujibu wa taarifa ya umoja wa Afrika kiasi cha mabinti milioni 14 barani humo huolewa kila mwaka wakiwa na umri mdogo na nyingi ya ndoa hizo zikiwa ni za kulazimishwa na wazazi wao.

Ndoa za utotoni zinakwenda kinyume na haki za binadamu na ,kumnyima haki ya kuwa na afya bora mtoto wa wa kike ikiwa ni pamoja na kumpa uhuru wa kufanya maammuzi ya kuolewa na nani na wakati gani aamue kufunga ndoa. Kikao hicho cha siku mbili kitawashirikisha wajumbe kutoka mataifa wanachama wa umoja huo wakiwemo wake wa maraisi na wawakilishi wa asasi mbalimbali za kiraia.

Msumbiji ni miongoni mwa mataifa yanayokabiliwa na changamoto hizo za ndoa za utotoni ambapo mfano mmoja wapo ni wa binti Lucia Felix mwenye umri wa miaka 15, anaetamani kuendelea na masomo katika shule iliyoko kijijini mwake, lakini bado anakabiliwa na changamoto ya uzazi kwani kabla ya kufanya hivyo inabidi kwanza ajifungue baada ya kupata uja uzito katika ndoa ambayo ilikuwa ya kulazimishwa.

Binti huyu ni miongoni ya mamilioni ya mabinti barani Afrika ambao wanaolewa katika umri mdogo na baadhi ya ndoa hizo zikiwa ni za kulazimishwa. "Siku moja kijana mmoja alifika hapa kijijini kwetu kuchagua mwanamke wa kuoa na alinichagua mimi, na hivyo baadaye nikashika mimba," binti huyo aliliambia shirika la habari la AFP wakati alipokuwa ameketi chini ya mti wa mwembe katika makazi ya familia yake yaliyoko katika kijiji cha Jangamo kusini mwa nchi hiyo.

Umaskini walazimisha wazazi kutoa mabinti

Lucia ambaye ana uja uzito wa miezi minane alikuwa ametoka tu kumuona daktari baada ya kuugua malaria na alikuwa akilalamika kusikia maumivu. "Ninaogopa kwa sabababu mie bado nina umri mdogo kiasi cha kuweza kumtunza vizuri mtoto na pia nataka kurudi shule na kuendelea na masomo kwani nataka niwe mwalimu hapo baadaye" alisema binti huyo.

Familia zinazoishi katika mazingira duni NigeriaPicha: DW/A. Kriesch

Mama mzazi wa binti Lucia aitwaye Zaide Zunguze anakiri kuwa aliunga mkono suala la uchumba kati ya Lucia na mtu aliyetaka kumuoa lakini alishauri hadi binti yake afikishe umri wa miaka 18 ndipo aweze kufunga ndoa na mchumba wake huyo mwenye umri wa miaka 20.

"Binti yangu bado ana umri mdogo hajui kitu kuhusiana na masuala ya ndoa, nilihitaji kuendelea kufundisha jinsi ya kutunza familiaa ni na ogopa kwa sababu muoaji aliahidi kumtunza mtoto lakini hadi sasa haonyeshi kutoa kauli yoyote," alisema mama mzazi wa binti huyo.

Umri halali wa kisheria wa mtu kuweza kuolewa nchini Msumbiji ni miaka 18 au 16 kwa ridhaa ya wazazi lakini karibu nusu ya mabinti nchini humo wanaolewa katika ndoa za kimila kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 na kwa mujibu wa sensa iliyopita nchini humo ya mwaka 2011 karibu asilimia 14 ya mabinti nchini humo wanaolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 15. "Suala la utoto hapa linatizamwa kitofauti kabisa, mara tu wanapoanza kuonyesha dalali za kuvunja ungo wanachukuliwa kuwa ni watu wazima," alisema Pascoa Ferrao ambaye ni mkurugenzi wa idara inayohusika na masuala ya kijamii nchini humo.

Aliongeza ya kuwa suala la ndoa za utotoni mara nyingi linahusishwa na sababu za kiuchumi kwani binti anapoozeshwa inakuwa tayari amepunguza mzigo wa matumizi ndani ya familia.

Hata hivyoalisema hali hii huchangia vifo vya watoto kwa sababu mabinti wenye umri chini ya miaka 18 hawana uwezo wa kuweza kuwatunza watoto wanao wazaa vizuri. Mataifa mengine yanayokabiliwa na changamoto ya ndoa za utotoni barani Afrika ni pamoja na Niger, Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mkutano huo wa Lusaka nchini Zambia utajikita zaidi katika kubadilishana uzoefu juu ya kujaribu kupunguza ndoa za utotoni barani humo.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman