1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika na matukio mapya nchini Chad.

6 Mei 2009

Ni baada ya Waasi kuanza harakati mpya za kijeshi

Rais wa Idriss Deby, (mwenye miwani)Picha: AP

Umoja wa Afrika umeelezea wasi wasi wake mkubwa kuhusiana na hatua ya kusonga mbele kwa waasi wa Chad wanaoungwa mkono na nchi jirani yake Sudan na ambayo inahujumu jitihada za hivi karibuni za kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya nchi hizo mbili.

Taarifa ya Umoja wa Afrika iliotolewa katika makao yake makuu mjini Addis Ababa, imesema kwamba Mwenyekiti wa tume ya umoja huo Jean Ping ,anafuatilia kwa wasi wasi mkubwa matukio ya hivi karibuni katika sehemu ya mashariki mwa Chad, baada ya kupatikana ripoti za kuwepo kwa harakati za waasi wenye silaha katika eneo hilo.

Taarifa hiyo ikaongeza kwamba Bw Ping amezitaka pande zote zinazohusika kujizuwia na hatua yoyote itakayozusha mgogoro na kuonyesha hali ya kuwajibika kwa manufaa ya Chad na eneo hilo kwa jumla.

Waasi hao waliingia ndani ya ardhi ya Chad wakiwa katika magari chungu nzima tangu siku ya Jumatatu katika kile kinachoonekana kuwa ni hatua ya kijeshi ya kujaribu kusonga mbele zaidi , wakisemekana walikua wakikaribia mji mmoja muhimu wa mashariki .

Waasi mashariki mwa ChadPicha: picture-alliance/dpa

Bw Ping amesema katika taarifa hiyo kwamba matukio haya ni jambo la kusikitisha mno na yametokea katika wakati ambao ni hivi majuzi tu Sudan na Chad zilitiliana saini makubaliano ya kuondoa hali ya uhasama na kurejesha uhusiano wa kawaida kati yao, katika mazungumzo yaliofanyika mjini Doha-Qatar na kuhudhuriwa na Mawaziri wanaohusika na uhusiano wa kimataifa wa nchi hizo mbili.

Wachambuzi wanasema makubaliano hayo yaliopatikana kutokana na upatanishi wa Qatar na Libya na kusainiwa Jumapili iliopita ni muhimu katika kufikiwa hatimae suluhisho lolote la kudumu la mgogoro wa miaka sita hivi sasa katika jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur.

Taarifa ya Mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika Bw Ping juu ya wasi wasi uliopo kuhusiana na hali hii mpya ilioripotiwa, imekuja siku moja baada ya kuripotiwa mapigano kati ya waasi hao na majeshi ya serikali ya Chad katika mkoa wa kusini mashariki wa salamat, huku waasi wakidai walikua wakijaribu kusonga mbele kuelekea mji mkuu Ndjamena.

Mjini Paris waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Bernard Kouchner alikutana na mwenzake wa Chad Moussa Faki Mahamat jana kuijadili hali ya mambo nchini Chad. Ufaransa ina wanajeshi 1.100 katika koloni lake hilo la zamani ikiwa ni chini ya mkataba kati ya nchi hizo mbili na wanajeshi wake 800 ni sehemu ya kikosi cha umoja wa mataifa kilichochukua nafasi ya kile cha umoja wa Ulaya mwezi uliopita kuwalinda wakimbizi katika makambi nchini humo, wengi wakiwa ni wale kutoka Darfur.

Wakimbizi kutoka DarfurPicha: AP

Chad imeishutumu mara kwa mara Sudan kuwa inawaunga mkono waasi wanaotaka kumuangusha Rais Idris Deby Itno, wakati ambapo Sudan kwa upande wake imeishutumu Chad kuwa inawaunga mkono waasi katika jimbo la Darfur.

Mwezi Februari mwaka jana waasi walifanikiwa kusonga mbele hadi kwenye vitongoji vya mji mkuu wa Chad Ndjamena katika jaribio lao la kutaka kumuangusha rais Derby, kabla ya shambulio lao kuzimwa kwa msaada wa wanajeshi wa Ufaransa walioko nchini humo, na waasi kuilaumu Ufaransa kwa kumsaidia kiongozi huyo ambaye wanasema ni dikteta anayekandamiza hatua yoyote ya kuleta demokrasia nchini humo.

Wakati hali ikirejea tete kuwa tete nchini Chad, Ufaransa imesema ina wasi wasi juu ya usalama wa raia.

Mwandishi:Mohamed Abdul-Rahman /AFPE

Mhariri:Aboubakary Liongo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW