1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika unakutana kujadili mgogoro wa Niger

14 Agosti 2023

Umoja wa Afrika umesema unafanya mkutano kuhusu mgogoro wa Niger kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya Julai 26 yaliyomuondowa madarakani rais Mohamed Bazoum.

Ägypten - Sudan - Summit
Picha: Egyptian Presidency Media Office/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa ujumbe ulioandikwa kwenye ukurasa wa Twitter na Umoja huo,baraza la amani na usalama la taasisi hiyo linakutana kupokea taarifa kuhusu hali iliyopo katika mgogoro wa Niger na juhudi za kulishughulikia suala hilo.Mkutano huo unafanyika katika makao makuu ya Umoja wa Afrika,mjini Addis Ababa nchini Ethiopia na miongoni mwa wanaohudhuria ni pamoja na mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja huo Mousa Faki Mahamat pamoja na wajumbe kutoka Niger na Jumuiya ya nchi za ushirikiano wa kiuchumi za Afrika Magharibi,ECOWAS.Mkutano huo umekuja wakati ambapo jana Jumapili utawala wa kijeshi wa Niger umesema utamfungulia mashtaka rais wanayemshikilia Mohamed Bazoum kwa kile ilichokiita uhaini wa kiwango cha juu. Utawala huo pia umekosoa vikwazo vilivyowekwa na ECOWAS dhidi ya nchi yake.