Umoja wa Afrika unataka kubadili mtazamo wake dhidi ya Libya
17 Januari 2012Akizungumza na Shirika la Habari la Ufaransa AFP, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jean Ping alijinasibu kwa kusema" Kile nilichoiambia serikali ya Libya kwanza ni kwamba kilichopita kimepita, pasipo kujali kilichotokea"
Katika mahojiano yake hayo aliongeza kusema lazima tubadili kurasa na kuangazia maendeleo.
Umoja wa Afrika ulitambua uongozi mpya wa Libya Septemba mwaka jana, baada ya kushindwa kusuluhisha mgogoro kati waasi na Gaddafi, ambae ni muasisi wa umoja huo.
Waasi ambao walikuwa wakiungwa mkono na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, walikataa mpango wa mazungumzo ulioratibiwa na AU wakionesha hali ya kutokuwa na uhusiano mzuri na umoja huo.
Lakini katika mahojiano haya ya sasa Ping alisema amekwenda Tripoli kwa ajili ya kuzungumza na serikali hiyo mpya juu ya mustakabali wa zama mpya za taifa hilo.
Kiongozi huyo wa juu wa Umoja wa Afrika aliongeza kusema utawala uliopita, ulikuwa na mbinu zake, vyanzo tofauti na mitazamo mengine dhidi ya mataifa tofauti kwa hivyo anafikiri kwamba utawala mpya utahitaji kuwa na ushirikiano wa kawaida na ndugu zake na Afrika kwa ujumla.
Alisema uhusiano wa taifa hilo na mengine ya jirani unakuwa kwa kasi, kwa haraka sana na katika mkondo sahihi huku akiahidi kustawisha uhusiano huo. Ping alidokeza kuwa Waziri Mkuu wa Libya Abdel Rahim al-Kib ambae alifanya nae mazungumzo hiyo jana, atahudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika unaotarajiwa kufanyika mjini Addis Ababa mwishoni mwa mwezi huu.
"Mfalme wa Wafalme" kama alivyopendwa kuitwa, hayati Kanal Gaddafi alikuwa muhusika katika uanzishwaji wa Umoja wa Afrika na kuongoza kampeni kali katika kuundwa Jumuiya ya Mataifa ya Afrika yeye akiwa na ndoto ya kuongoza jumuiya huyo.
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika alisema kulikuwa na mjadala mkubwa juu ya kasi ya uundwaji wa Jumuiya hiyo, huku baadhi ya mataifa yakitaka mchakato wake ufanyike taratibu na mengine yakihimiza kasi ya kufikiwa kwa hatua hiyo.
Alisema anatarajia kwamba mjadala utaendelea hata baada ya kifo cha Gaddafi ambae aliuwawa na waasi Oktoba 20 huko maeneo ya karibu na mji aliozaliwa wa Sirte. Lakini aliongeza kwamba tofauti na awali mazungumzo ya sasa hayatakuwa na shinikizo la Gaddafi ambae alikuwa kitaka kutimiza ndoto yake.
Ping alionesha kupuuzia nguvu za utawala wa Gaddafi katika Umoja wa Afrika ikiwemo kiuchumi kwa kusisitiza kwamba kiongozi huyo hakuwa mfadhili mkuu wa umoja huo.
Alitaja mataifa mengine ambayo yalikuwa yakitoa mchango mkubwa sawa na Libya wa kiasi cha asilimia 15 kuwa Algeria, Misri, Nigeria na Afrika Kusini huku asilimia nyingine 25 zikipatikana kwa mataifa mengine.
Mwandishi: Sudi Mnette//AFP
Mhariri: Yusuf Saumu