1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika leo waanza mikutano miwili ya kilele

John Juma Mhariri: Iddi Ssessanga
27 Mei 2022

Wakuu wa nchi 20 pamoja na wafadhili wanashiriki kwenye mkutano huo wa kilele wa kwanza na wa kipekee unoalenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kushughulikia mizozo.

Äthiopien | AU Gipfel in Addis Abeba | Mohammed Schtajjeh
Picha: Shadi Hatem/APA Images/ZUMAPRESS/picture alliance

Kulingana na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat, Waafrika wapatao milioni 113 wanahitaji misaada kwa haraka mwaka huu, wakiwemo wahamiaji milioni 48, wanaotafuta hifadhi katika mataifa mengine na vilevile wakimbizi wa ndani.

Mkutano wa pili wa kilele utafanyika kesho Jumamosi ambapo viongozi watajadili masuala ya ugaidi, mabadiliko yasiyo ya kikatiba, wakati ambapo bara la Afrika linakabiliwa na machafuko yanayoendeshwa na makundi ya itikadi kali katika nchi za Libya, Msumbiji, Somalia, kanda ya Sahel, magharibi mwa Ziwa Chad na katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki MahamatPicha: Giscard Kusema/Press Office Presidency of DRC

Kwenye taarifa, Umoja wa Afrika umesema nchi 15 ambazo zimeathiriwa mno zinahitaji misaada ya dharura hasa wakati huu ambao athari za mabadiliko ya tabia nchi zinafanya mahitaji ya kibinadamu kuongezeka kwa kiwango kikubwa.

Umoja huo umeongeza kuwa miongoni mwa watu milioni 30 ambao wamepoteza makaazi yao, zaidi ya milioni 10 ni Watoto walio na miaka chini ya 15, ukitaja mizozo ya kikabila katika baadhi ya kanda na vilevile tatizo la ukosefu wa upatikanaji wa chakula.

Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO - limesema takriban watu milioni 282 miongoni mwa idadi jumla ya watu barani Afrika Bilioni 1.4, hawapati chakula cha kutosha. Hiyo ikiwa ni ongezeko la watu milioni 49 tangu mwaka 2019.

Wakulima nchini MsumbijiPicha: Bernardo Jequete/DW

Katika miaka miwili iliyopita, mapinduzi ya kijeshi nchini Mali, Guinea, Sudan na Burkina Faso yamesababisha jeshi kuwang'oa madarakani marais waliochaguliwa, kisha wakaweka utaratibu wa muda mrefu wa kurejesha utawala wa kiraia.

Matukio hayo yamelaaniwa vikali na vikwazo pia kuwekwa na miungano ya kikanda, mfano Umoja wa Ulaya na nchi za magharibi. Isitoshe Umoja wa Afrika ulifuta uanachama wa mataifa manne hadi pale watawala wa kijeshi watakaporejesha utawala kwa raia.

Kulingana na Mahamat, mapinduzi yanaashiria kurudi nyuma kwa michakato ya kidemokrasia ambayo nchi zimekuwa zikiendeleza kwa miongo miwili iliyopita.

Alivitaja vipindi vya mpito ambavyo vimewekwa na watawala wa kijeshi kuwa ‘vyanzo vya mafarakano na mivutano ya mara kwa mara' visivyofaa kwa utulivu wa mataifa yenyewe na majirani zao.

Mahamat amesema huenda baadhi ya mataifa yakaitaja Chad kama kisingizio, ambayo tangu Aprili 2021, imetawaliwa na Jenerali Mahamat Idriss Deby, mwanaye kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Idriss Deby Into.

Baada ya Deby kuahidi kuandaa uchaguzi huru na wa kidemokrasia ndani ya miezi 18 kufuatia mjadala wa kitaifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Ufaransa, zilimuunga mkono Deby, hata ingawa zililaani tawala za kijeshi kwingineko.

Aliyekuwa rais wa Chad marehemu Idriss DebyPicha: Brahim Agji/AFP/Getty Images

Lakini mazungumzo ya awali nchini Qatar kati ya serikali na makundi ya waasi yamekwama na vilevile yamesusiwa na vyama vya upinzani hivyo kusababisha mazungumzo kamili na uchaguzi kuahirishwa.

Tayari Deby ametangaza uwezekano wa kurefusha kipindi cha mpito kwa miezi mingine 18.

Chanzo/AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW