1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGabon

Umoja wa Afrika wasimamisha uanachama wa Gabon

1 Septemba 2023

Umoja wa Afrika, umesimamisha uanachama wa Gabon baada ya mapinduzi ya kijeshi katika taifa hilo la Afrika ya Kati. Umoja huo umesimamisha ushiriki wa Gabon katika shughuli zake na taasisi zake zote mara moja

Viongozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika katika picha ya pamoja wakati wa kikao cha kawaida cha 35 cha Umoja huo mjini Addis Ababa nchini Ethiopia mnamo Februari 5, 2022
Viongozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika katika picha ya pamoja wakati wa kikao cha kawaida cha 35 cha Umoja huoPicha: Amanuel Sileshi/AFP

Siku ya Alhamisi (31.08.2023) baraza la amani na usalama la Umoja huo, lilisema kuwa linalaani vikali mapinduzi hayo yaliomuondoa madarakani rais Ali Bongo. Wiki chache zilizopita, Umoja huo wa Afrika pia ulisimamisha uanachama wa Niger baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Julai.

Soma pia:Umoja wa Ulaya wasema hakuna mipango ya kuwaondoa raia wa nchi za umoja huo kutoka Gabon.

Uanachama wa Burkina Faso, Mali, Guinea na Sudan katika Umoja huo pia umesimamishwa tangu mapinduzi ya kijeshi katika mataifa hayo.

Umoja wa Ulaya unapinga mapinduzi ya kijeshi nchini Gabon

Katika hatua nyingine, mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amesema kuwa Umoja huo unapinga kutwaliwa kwa nguvu kwa mamlaka nchini Gabon. Katika taarifa hapo jana, Borrell amesema kuwa changamoto zinazoikabili Gabon lazima zitatuliwe kulingana na kanuni za sheria, utaratibu wa kikatiba na demokrasia.

Ali Bongo, Rais wa Gabon aliyeondolewa madarakani Picha: TP advisers on behalf of the President's Office/AP Photo/picture alliance

Soma pia:Viongozi wa Afrika kujibu hatua ya mapinduzi ya kijeshi Gabon

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa amani na ustawi wa taifa hilo pamoja na utulivu wa kikanda unategemea masuala hayo. Borrell ametoa wito wa mazungumzo jumuishi na madhubuti badala ya nguvu ili kuheshimu utawala wa sheria, haki za binadamu na matakwa ya raia wa Gabon.

Maafisa wa jeshi watangaza kuvunjwa kwa taasisi zote za serikali

Jeshi lilipindua serikali ya Gabon mapema Jumatano (30.08.2023). Maafisa wa jeshi hilo walitangaza kupitia televisheni ya taifa kwamba taasisi zote za serikali zimevunjwa, matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni kufutwa kwasababu ya dosari za uchaguzi na mipaka ya nchi hiyo kufungwa.

Soma pia:Ufaransa, Uingereza na Umoja wa Afrika walaani mapinduzi ya kijeshi Gabon

Muda mfupi kabla ya mapinduzi hayo, maafisa wa uchaguzi walikuwa wamemtangaza Bongo ambaye amekuwa uongozini tangu mwaka 2009, mshindi wa uchaguzi huo wa Agosti 26. Jumatano jioni, viongozi wa kijeshi, walimtaja mkuu wa ulinzi wa rais Brice Clotaire Oligui Nguema kama kiongozi wa mpito wa taifa hilo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW