Umoja wa Afrika wataka kujenga upya mfumo wake wa usalama
2 Machi 2009Ujerumani imeimarisha na kupanua juhudi zake kwa ajili ya kudumisha amani na usalama barani Afrika. Juhudi hizi zinajumulisha mafunzo kwa wanajeshi wa kulinda amani, polisi na miradi ya kuweka alama mipaka. Kuzuia kutokea kwa mizozo na kudumisha amani ni mambo muhimu katika sera za kigeni za serikali ya Ujerumani.
Changamoto hizi za sera za Ujerumani kuelekea bara la Afrika zilijadiliwa hivi majuzi mjini Berlin hapa Ujeruamni. Miongoni mwa wajumbe walioshiriki kwenye mkutano huo ni Ramtane Lamamra, kamishna anayehusika na maswala ya amani na usalama wa Umoja wa Afrika. Mjumbe huyo pamoja na wajumbe wa kisiasa wa Ujerumani walijadiliana kuhusu hatua zilizopigwa na Umoja wa Afrika katika mfumo wake wa usalama.
Amani na usalama havitakiwi kudumishwa baada ya mizozo barani Afrika. Kwa msingi huo Umoja wa Afrika unataka kujenga upya mfumo wake wa usalama kuhakikisha hili linatimia. Kudumisha amani barani Afrika hakuanzi na kuwapokonya silaha waasi au wanajeshi wala kuwatuma wanajeshi wa Umoja wa Afrika katika nchi fulani.
Ramtane Lamamra anasema kudumisha usalama na kutanzua mizozo kunahitaji kuzingatia mtu yeyote asilazimike kuhofu umaskini na kwamba elimu na huduma za afya zinapatikana. Haki msingi za binadamu lazima ziheshimiwe na katika swala hili Umoja wa Afrika unapaswa kuelewa maana ya usalama anasema bwana Lamamra.
"Lazima tuelewe maana pana ya neno usalama. Amani na usalama ina maana kuzuia mizozo pamoja na kazi ya kujenga upya baada ya mizozo kumalizika. Usalama unahusu ushirikiano, kuendeleza maendeleo na maingiliano ya bara zima. Inahusu maingiliano ya kiuchumi, hususan katika ngazi ya kikanda. Inahusu thamani ya pamoja ya misingi ya demokrasia, utawala bora, haki za binadamu na pia kujali haki msingi za kijamii. Na Waafrika kwa pmaoja wanatakiwa kujenga taasisi na kuimarisha kwa mfano bunge na mahakama ya Afrika."
Ndio maana Umoja wa Afrika haujatupilia mbali kanuni ya kutokuwa na maingiliano. Unatakiwa kuingilia kati wakati kunapotokea visa vya ukiukaji wa haki za binadamu. Baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika, ambalo bwana Lamamra ni mwanachama, huamua kupeleka wanajeshi wake katika maeneo ya mizozo na hudhaminiwa na benki ya dunia na Umoja wa Ulaya.
Bila msaada huu wa kifedha kutoka nje Umoja wa Afrika ungelemewa. Hata leo kunakosekana wanajeshi wa kutumwa kwenye maeneo ya vita kwa mfano tume ya Umoja wa Afrika nchini Sudan au Somalia. Nchini Somalia wanajeshi wa Uganda na Burundi walipelekwa ingawa idadi yao ni ndogo mno. Nchi za Afrika zinatakiwa zenyewe kutoa mchango zaidi anasema bwana Lammra, kamishna anyehusika na maswala ya amani na usalama wa Umoja wa Afrika.
"Waafrika wana jukumu la kuchangia gharama za shughuli za Umoja wa Afrika. Lakini kadri shughuli hizi zinavyopanuka, ndivyo inavyozidi kuwa muhimu kufanya mengi zaidi na hata kutoa michango zaidi. Inahusu maingiliano na maendeleo ya bara zima. Afrika inatakiwa kubeba jukumu la kujikwamua yenyewe na hii ina maana kuendelea kukua kwa tume za Umoja wa Afrika."
Kwa sababu hiyo Umoja wa Afrika unataka kuunda kikosi cha akiba kitakachojumulisha maafisa wa polisi na raia kufikia mwaka 2010. Kila eneo kati ya maeneo matano linatakiwa kuwa na kikosi chake ambacho kwa haraka kitakakuwa kikibiliana na mizozo wakati itakapotokea.
Ulaya imeahidi kuisadia Afrika kwenye mkutano wake uliofanyika mjini Lisbon nchini Ureno mnamo mwaka 2007 kwa kuwa amani ya Afrika ni muhimu kuhakikisha ushirikiano. Umoja wa Ulaya unadhamini tume za Umoja wa Afrika kwa kiwango cha yuro milioni 300 na fedha hizo zinatakiwa kutumika moja kwa moja katika tume za umoja huo nchjini Sudan, Somalia na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Akizungumzia kuhusu tume ya Umoja wa Afrika nchini Somalia bwana Lamamra amesema umoja huo umeingia nchini humo kwa lengo la kusaidia na wala si vinginevyo.
"Nina matumaini makubwa sana kwamba viongozi wa Somalia wanaelewa kuwa Umoja wa Arfrika na wanajeshi wake wamo nchini humo kuwasaidia. Hii si mamlaka inayotaka kuikalia Somalia. Lakini ni wazi kwamba tume yetu nchini humo itamalizika mara tu Wasomali wenyewe watakapofahamu umuhimu wa kujenga tena taasisi za serikali zilizo imara."
Umoja wa Afrika umefaulu kuleta utulivu nchini Burundi na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Umefaulu pia kuendesha uchaguzi nchini Ivory Coast. Somalia bado ni eneo tete kwa baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika na bwana Lamamra anaukosoa uongozi wa Somalia kwa kutokuwa na ari ya kisiasa kudumisha amani nchini humo.