1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yatoa wito wa hatua za haraka kuchukuliwa Mali

10 Novemba 2025

Umoja wa Afrika umetoa wito wa kuchukuliwa hatua haraka ya kimataifa, ikiwemo ushirikiana wa kutoa taarifa za kijasusi ili kushughulikia hali mbaya ya kiusalama nchini Mali.

Addis Ababa 2025 | Umoja wa Afrika | Mahmoud Ali Youssouf
mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali YoussoufPicha: Amanuel Sileshi/AFP/Getty Images

Katika taarifa yake, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, alielezea wasiwasi wake kuhusu hali halisi inayoendelea Mali, ambako kundi la wanamgambo wa Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM),limeweka vizuizi  vya uingizwaji mafuta tangu mwezi Septemba, kutatiza kufikiwa kwa mahitaji muhimu na kuzidisha hali mbaya ya kibinaadamu kwa watu wa taifa hilo.

Amependekeza kwamba kunapaswa kuwa na ushirikiano wa hali ya juu wa taarifa za kijasusi kwa mataifa yaliyo katika Ukanda wa Sahel yaliyoathiriwa na hujuma za makundi ya wanamgambo walio na itikadi kali huku akisisitiza kuwa Umoja wa Afrika uko tayari kuiunga mkono Mali pamoja na eneo zima la Sahel katika wakati huu mgumu, bila ya kutoa ufafanuzi zaidi juu ya hilo.

Mahmoud Ali Youssouf,  pia ametoa wito wa kuachiwa mara moja raia watatu wa Misri waliotekwa  hivi karibuni na kundi hilo la wanamgambo. Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin imekuwa ikiwalenga raia wa kigeni ili kupata fedha za kuendeleza operesheni zake Magharibi mwa Afrika.

Matendo ya wanamgambo wa Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM)  yameibua wasiwasi kwamba huenda wakajaribu kulazimisha utawala wao nchini Mali.Picha: Reuters

Shirika la habari la Reuters liliripoti mwezi Oktoba kwamba makubaliano yalifikiwa ya wanamgambo kuwaachia raia wawili Umoja wa Falme  za kiarabu UAE baada ya kudai kikomboleo cha dola milioni 50.

JNIM huenda wakalazimisha utawala wao Mali

Wanamgambo hao walioko katika eneo la Sahel Magharibi mwa Afrika na walio na mafungamano na kundi la kigaidi la Al Qaeda, walitangaza kuzuia uagizaji huo wa mafuta katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi isiyo na bandari, na tangu wakati huo wamekuwa wakishambulia misafara ya malori ya mafuta yanayojaribu kuingia nchini humo.

Hali hiyo imesababisha uhaba mkubwa wa mafuta na kulazimisha shule na vyuo vikuu kufungwa kwa wiki kadhaa.

Hatua hii inatajwa na wachambuzi kuwa ni sehemu ya kampeni ya makundi hayo ya wanamgambo inayolenga kuzidisha shinikizo kwa serikali ya kijeshi ya Mali kwa kuzuwia na kulemaza chanzo kikuu cha uchumi nchini humo.

Matendo ya wanamgambo hao wa Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM)  yameibua wasiwasi kwamba huenda hatimae wakajaribu kulazimisha utawala wao nchiniMali. Haya yanajiri wakati mataifa ya Magharibi yakiwemo Marekani, Ufaransa, Uingereza na Italia yanawahimiza wananchi wao kuondoka nchini humo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW