1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UAE yakubali kusambaza gesi na dizeli nchini Ujerumani

26 Septemba 2022

Umoja wa Falme za Kiarabu umekubali kusambaza gesi asilia na dizeli kwa Ujerumani kama sehemu ya makubaliano ya "usalama wa nishati" kuchukua nafasi ya bidhaa za Urusi.

Bundeskanzler Scholz mit Emir Von Katar Tamim bin Hamad Al Thani
Picha: Qatar News Agency/AP/picture alliance

Scholz alitia saini mkataba huo akiwa katika ziara ya Ghuba iliyompeleka katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia na Qatar kutafuta vyanzo vipya vya nishati. Scholz alikutana na rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohamed bin Zayed Al-Nahyan, ambaye kupitia mtandao wa twitter amesema kuwa walizungumza kuhusu ushirikiano katika maeneo yanayohusu usalama wa nishati na hatua za hali ya hewa.

Shirika la habari la Umoja wa Falme za Kiarabu WAM limeripoti kuwa kiongozi huyo wa Ujerumani amepongeza makubaliano hayo ya usalama wa nishati. WAM imeripoti kuwa shirika la mafuta la Umoja wa Falme za Kiarabu ADNOC limekamilisha usambazaji wake wa kwanza wa dizeli wa moja kwa moja nchini Ujerumani mwezi huu, na litasambaza hadi tani 250,000 za dizeli kwa mwezi mnamo mwaka 2023.

Tani za kwanza za gesi kusambazwa Ujerumani mwezi Desemba

Katika taarifa, Kampuni ya nishati ya RWE imesema kuwa tani 137,000 za kwanza za gesi asilia iliyoyeyuka zitasambazwa mwezi Desemba katika kituo kipya cha Ujerumani cha uagizaji kutoka nje na usambazaji wa gesi asilia iliyoyeyuka -LNG- huko Brunsbuettel, karibu na Hamburg.

Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman Picha: SAUDI PRESS AGENCY/VIA REUTERS

Ziara ya siku mbili ya Scholz katika Ghuba ililenga kusaini mikataba mipya ya nishati kuchukua nafasi ya usambazaji wa Urusi na kupunguza mzozo wa nishati uliotokana na uvamizi wa Moscow nchini Ukraine. Siku ya Jumamosi, Scholz alikutana na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman huko Jeddah.

Hakuna mikataba iliyotangazwa Qatar

Kulingana na taarifa rasmi, Jumapili alasiri, alifanya mazungumzo huko Doha na kiongozi wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani kuhusu nishati na uwekezaji. Hata hivyo hakuna mikataba iliyozangazwa nchini Qatar.

Scholz amesema rekodi yenye utata ya haki nchini Qatar inaimarika lakini hakutoa hakikisho la kuhudhuria michuano ya kombe la dunia katika taifa hilo la ghuba inayoanza mwezi Novemba. Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia na Qatar zimekuwa wakosoaji wa kile wanachokiita mifumo ya mpito ya nishati isiyo halisi ambayo wanasema imechangia katika uhaba ambao umelikumba bara Ulaya katika muda wa miaka miwili iliyopita. Akiwa Abu Dhabi, Scholz amewaambia wanahabari kwamba nchi yake imepiga hatua katika mfululizo wa miradi kwa upande wa uzalishaji na ununuzi wa dizeli na gesi, huku akiongeza kuwa ilidhamiria kuzuia utegemezi wa nishati kwa Urusi.

 

     

     

  

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW