Umoja wa Mataifa: Dola bilioni 3 zahitajika kuisaidia Sudan
17 Mei 2023Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa lilaloratibu msaada wa kibinaadamu, UNOCHA, Ramesh Rajasingham amesema Jumatano kuwa mahitaji yameongezeka tangu mapigano yalipozuka Sudan Aprili 15.
Watu milioni 25 wanahitaji msaada
Akizungumza na waandishi habari mjini Geneva, Ramesh amesema watu milioni 25, ambao ni zaidi ya nusu ya wananchi wa Sudan wanahitaji msaada wa kiutu na ulinzi.
"Mpango huu tunaouzindua leo unaonesha ukweli uliopo. Kupitia mpango huu, ambao ni mpango wa kila mwaka wa mwitikio wa kibinadamu wa 2023 uliorekebishwa, tunalenga kuwafikia watu milioni 18," alifafanua Ramesh.
Mkuu huyo wa shirika la UNOCHA amesema kuwa mahitaji ya Sudan ni ya muhimu na yanaongezeka kama inavyotarajiwa kwenye mizozo na kwamba panahitajika msaada wa matibabu, chakula, maji, malazi, usafi na huduma ya kukabiliana na kiwewe.
Kwa mujibu wa Ramesh, pia wamepokea taarifa zenye kuleta wasiwasi za kuongezeka kwa unyanyasaji wa kingono, huku wahanga wakiwa hawapati msaada.
Watu wapatao 1,000 wameuawa
Mapigano kati ya majenerali wawili wanaogombania madaraka nchini Sudan, yamesababisha mauaji ya takribani watu 1,000, hasa kwenye mji mkuu, Khartoum pamoja na kwenye eneo la magharibi mwa jimbo la Darfur.
Mapigano hayo yamezidisha mzozo wa kiutu Sudan ambako tayari mtu mmoja kati ya watatu alikuwa akitegemea msaada hata kabla ya vita kuanza.
Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR, limesema dola milioni 470.4 zitahitajika kwa ajili ya kuwasaidia watu wanaokimbia Sudan, likiongeza kuwa linatarajia hadi watu milioni 1.1 watavuka mpaka wa Sudan mwaka huu pekee.
Makamu Mkuu wa operesheni za UNHCR, Raouf Mezou amewaambia waandishi habari kwamba hadi sasa, mzozo huo umesababisha wimbi kubwa la watu kukimbilia kwenye nchi jirani, ambako kiasi ya wakimbizi 220,000 na waliorejea wamekuwa wakitafuta usalama nchini Chad, Sudan Kusini, Misri, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Ethiopia.
Wiki mbili zilizopita, UNHCR ilisema itahitaji dola milioni 445 ifikapo mwezi Oktoba, kwa ajili ya kushughulikia majitahi ya watu 860,000 ambao wanaweza kuikimbia nchi hiyo. Aidha, zaidi ya watu 700,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani.
Mezou amesema watu wasiohesabika bado wamekwama ndani ya Sudan na wale ambao wamekimbia kuvuka mipaka mara nyingi wanawaacha nyuma ndugu zao au wengine wanakufa na kujikuta katika maeneo ambayo sio rahisi kuyafikia, huku rasilimali zikiwa ndogo.
(AFP, Reuters)