1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa kujadili haki za binadamu Ethiopia

14 Desemba 2021

Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa limesema litaandaa kikao maalum kwa ajili ya kuijadili hali ya haki za binaadamu nchini Ethiopia baadae wiki hii.

Tigray-Konflikt | Flucht in den Sudan
Picha: ASHRAF SHAZLY/AFP

Mkutano huo utafanyika kutokana na ombi la Umoja wa Ulaya ambalo limeungwa mkono na zaidi ya nchi 50. Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa uamuzi kuhusu mkutano huo utakaofanyika siku ya Ijumaa umekosolewa vikali na serikali ya Ethiopia.

Umoja wa Ulaya ulisema jana kwamba jumuia ya kimataifa ina wajibu wa kuzuia ukatili zaidi na kuhakikisha waathirika wanapata haki yao na wahusika wanachukuliwa hatua. Balozi wa Umoja wa Ulaya katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Lotte Knudsen amesema kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya, jumuia ya kimataifa inapaswa kujaribu kukomesha ukiukaji wa haki za binaadamu.

Azimio la Umoja wa Ulaya

Rasimu ya azimio la Umoja wa Ulaya iliyowasilishwa inalaani ukiukaji unaofanywa na pande zote zinazohasimiana katika mzozo wa kaskazini mwa Ethiopia kwenye jimbo la Tigray, ambao mkuu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet alisema mwezi uliopita kwamba unaweza kuwa uhalifu wa kivita.

Iwapo itapitishwa inaweza kuchangia kuundwa kwa tume ya wataalamu wa kimataifa kuchunguza zaidi ukiukaji wa haki za binadaamu nchini Ethiopia na kutoa ripoti yao baada ya mwaka mmoja. Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amesema anasikitishwa na kile alichoeleza kwamba umoja huo umeshindwa kukubaliana kuhusu vikwazo ambavyo amesema huenda vingesaidia kupunguza baadhi ya ukiukwaji.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep BorrellPicha: Alexey Vitvitsky/Sputnik/picture alliance

''Ninakiri kwamba Ethiopia ni moja ya masuala ambayo tumejadili sana mwaka huu. Na pia ni moja ya masikitiko yangu makubwa kwa sababu tumeshindwa kuchukua hatua ipasavyo kuzuia ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Tumeshindwa kuzuia, kutokana na kukosekana kwa umoja katika baraza,'' alifafanua Borrell.

Borrell ameuambia mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, kwamba wameshindwa kuzuia ubakaji, unyanyasaji wa kingono unaotumika kama silaha ya kivita, mauaji pamoja na kambi za mateso.

Ethiopia yawataka wajumbe kususia

Wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia iliwataka wanachama wa baraza hilo kukataa kupiga kura kwa ajili ya kikao maalum na matokeo yake yaliyochochewa kisiasa. Msemaji wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, amesema kutokana na kikao hicho maalum kuungwa mkono na zaidi ya theluthi moja ya nchi wanachama 47 wa baraza hilo, hakuna njia Ethiopia inaweza kuzuia usifanyike. Hata hivyo, wanachama wanaweza bila shaka kupiga kura kulipinga azimio hilo.

Malefu ya watu wameuawa katika vita vya Ethiopia vilivyozuka Novemba mwaka uliopita kati ya vikosi vya serikali na vikosi vya chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, mapigano hayo yamesababisha zaidi ya watu milioni mbili kuyakimbia makaazi yao na maelfu wengine kukumbwa na baa la njaa.

(AP, AFP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW