Umoja wa Mataifa kupeleka maafisa zaidi Somalia
11 Agosti 2010Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Somalia, Augustine Mahiga, anataraji kwamba tume anayoingoza itawapeleka wafanyakazi wa kimataifa katika maeneo ya Somalia yaliyojitenga ya Puntland na Somaliland, katika kipindi cha miezi kadhaa ijayo. Hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa, Martin Nesirky.
Mahiga amesema ni muhimu kwa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya kisiasa kwa ajili ya Somalia, hatimaye iwe na wajumbe wake katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, ambao hivi sasa ni uwanja wa mapiganao kati ya wanajeshi wa serikali na wanamgambo wa kiislamu. Lakini, hata hivyo, Mahiga ambaye ni balozi wa zamani wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, amesisitiza kuwa kwa sababu za kiusalama, tume hiyo ya Umoja wa Mataifa italazimika kufanya shughuli zake kwa uangalifu mkubwa.
Machafuko yameukumba mji mkuu wa Mogadishu tangu Umoja wa Afrika ulipowapeleka wanajeshi wake wa kulinda amani mnamo mwaka 2007 kuilinda serikali ya mpito ya Somalia dhidi ya wanagambo wa Kiislamu wanaoyadhibiti maeneo mengi ya nchi hiyo. Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, linawalisha watu 340,000 mjini Mogadishu, ambako idadi kubwa ya wakaazi wanaokabiliwa na kitisho cha kushambuliwa wanaishi.
Kwa sasa kuna wafanyakazi zaidi ya 60 wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, wakiwemo wafanyakazi 800 wa Kisomali, wanaofanya kazi na mashirika mbalimbali ya umoja huo. Kazi yao ni kuwapelekea misaada ya kibinadamu Wasomali, kuwasaidia kuondokana na athari za vita na kufanikisha miradi ya maendeleo inayonuiwa kuwanufaisha Wasomali takriban milioni 3.2.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alisema Jumatatu wiki hii kwa kuwa Umoja wa Afrika unakaribia kuwa na wanajeshi 8,000 wa kulinda amani nchini Somalia, Umoja wa Mataifa unatalia maanani kuwa na maafisa wake mjini Mogadishu na maeneo mengine yanayokabiliwa na vita nchini Somalia.
Wakati haya yakijiri, wanamgambo wa al Shabaab wameyapiga marufuku mashirika matatu ya misaada ya kikristo yasifanye kazi nchini Somalia kwa tuhuma kwamba yanawahubiria Wasomali wawe wakristo. Kundi la al Shabaab limeliamuru shirika la World Vision, Shirika la misaada la maendeleo la ADRA na shirika la Diakonia yakome mara moja kuendesha shughuli zao nchini Somalia. Taarifa ya al Shabaab imesema mashirika hayo yakijificha chini ya mwavuli wa mashirika ya kutoa misaada, yamekuwa yakieneza itikadi potofu.
Shirika la World Vision na ADRA yamethibitisha kusitisha harakati zao Somalia na kueleza kuwa yamevunjwa moyo na hatua hiyo ya al Shabaab. Shirika la Diakonie kutoka Sweden linalolodhaminiwa na makanisa matano halijatoa taarifa yoyote.
Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/DPAE
Mhariri: Othman Miraji