1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa: Mzozo wa kibinaadamu unanukia Ethiopia

27 Agosti 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelionya Baraza la Usalama la umoja huo, kwamba mzozo wa Ethiopia unasambaa nje ya Tigray na janga la kibinaadamu linajitokeza nchini humo.

UN-Generalsekretär António Guterres
Picha: Javier Soriano/AFP

Akizungumza jana na nchi 15 wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika kikao kilichokuwa kinaijadili hali katika jimbo la Tigray, Guterres amesema vitendo vya kichochezi na mzozo wa kibinaadamu vinaigawa jamii ya nchi hiyo. Amesema pande zote zinapaswa kumaliza uhasama mara moja bila ya kuweka masharti na kuitumia fursa hiyo kujadiliana kuhusu makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano.

''Mapambano ya kijeshi yaliyoanza takriban miezi 10 iliyopita kwenye jimbo la kaskazini la Tigray yanasambaa. Na kiwango cha binadamu wanaoteseka kinaongezeka huku kukiwa na athari kubwa za kisiasa, kiuchumi na kibinaadamu kwa Ethiopia na ukanda mkubwa. Pande zote zinapaswa kutambua hakuna suluhisho la kijeshi,'' alifafanua Guterres.

Guterres amesema mapambano ya kijeshi kwenye jimbo la Tigray yamefika hadi kwenye mikoa jirani ya Amhara na Afar. Amebainisha kuwa mzozo wa Tigray umesababisha zaidi ya watu milioni mbili kukosa makaazi na wanahitaji msaada, ikiwemo chakula, maji, malazi na huduma za afya na wengine 400,000 wanakabiliwa na kitisho cha njaa.

Wananchi wa Ethiopia waliokimbia vita Tigray wakisubiri kupewa chakulaPicha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Shrika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto, UNICEF, limeonya kuwa watu 100,000 wamekumbwa na utapiamlo mbaya ndani ya mwaka huu. Katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema mbali na Tigray, mzozo katika majimbo ya Afar na Amhara umesababisha zaidi ya watu 300,000 kukosa makaazi.

Guterres ataka uwajibikaji

Huku kukiwa na taarifa za kuwepo unyanyasaji wa kijinsia na kingono, kambi za wakimbizi zimeharibiwa na hospitali zimeporwa. Guterres amesema analaani vitendo hivyo vya kikatili, huku akitaka kuwepo uwajibikaji.

Kwa upande wake Marekani imesema serikali ya Ethiopia haijaitikia vya kutosha wito wa kufanyika mazungumzo na imeikosoa hatua ya majeshi ya Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF kujitanua hadi Afar na Amhara na vikosi vya ulinzi vya nchi jirani ya Eritrea kuingia tena Tigray. Naibu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Richard Mills amesema hali hiyo inatia wasiwasi, kwani matukio hayo yanadhoofisha uhuru, umoja na uadilifu kwenye jimbo hilo la Ethiopia.

Kiongozi wa TPLF, Debretsion GebremichaelPicha: DW/M. Haileselassie

Wakati huo huo, kiongozi wa vikosi vya Tigray, Debretsion Gebremichael ameelezea nia yake ya kufanya mazungumzo ya kumaliza vita. Katika barua yake aliyomuandikia Guterres, Debretsion amesema miongoni mwa masharti mengine, upande wa Tigray unahitaji mpatanishi asiye na upendeleo.

Umoja wa Afrika waonywa

Aidha, ameonya kuwa Umoja wa Afrika, ambao makao makuu yake yako Ethiopia hauwezi kutoa suluhisho lolote katika vita hivyo. Kauli hiyo inazifanya juhudi za umoja huo kumteua rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo kama mwakilishi wake maalum katika Pembe ya Afrika kuwa ngumu.

Taye Atske Selassie, Mwakilishi wa Kudumu wa Ethiopia katika Umoja wa Mataifa, amesema lengo lao ni amani, lakini kwa bahati mbaya TPLF inasimama kati ya Ethiopia na amani. Taye amesema TPLF sio mwathirika, ni mhalifu na watu wa Ethiopia, hasa Afara, Amhara na Tigray wanaishi katika mazingira wasiyostahili. Matarajio ya mazungumzo kati ya serikali ya Ethiopia na uongozi wa Tigray bado ni changamoto kubwa.

(AP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW