1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Umoja wa Mataifa: Mamilioni wakumbwa na njaa Sudan

11 Agosti 2023

Umoja wa Mataifa umesema mapigano ya Sudan yamesababisha baa la njaa kwa watu milioni 20.3.

Mzozo wa Sudan na baa la njaa
Tangu kuzuka mapigano nchini Sudan, hali ya upatikanaji chakula imekuwa ya taabu kwa mamilioni ya watu.Picha: Tony Karumba/AFP via Getty Images

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limesema leo kuwa kati ya wakaazi milioni 46 wa Sudan, takribani milioni 6.3 wanakabiliwa na uhaba wa chakula unaotishia maisha.

Mwakilishi wa WFP nchini Sudan, Eddie Rowe, amesema tangu kuzuka kwa mapigano mwezi Aprili, mzozo umesambaa na imekuwa vigumu kupeleka misaada ya kiutu. Rowe ametoa wito kwa pande zinazoahsimiana kuratibu upelekwaji wa misaada.

Wiki iliyopita, WFP ilifanikiwa kwa mara ya kwanza kupeleka chakula hasa kwenye jimbo lililoathiriwa zaidi la Darfur Magharibi, lililoko kwenye mpaka na Chad.

Rowe ameielezea hali katika majimbo ya Darfur Magharibi na katikati mwa Darfur kama ''janga,'' akisema kwamba wanaume wengi kwenye vijiji vya Darfur Magharibi walifariki dunia, walijeruhiwa au walitoweka, na kuziacha familia zao zikijitegemea zenyewe.