Umoja wa Mataifa umemkosoa rais wa Venezuela
30 Juni 2017Wito huo wa Umoja wa mataifa umetolewa wakati serikali ya Maduro ikiendelea kukandamiza maandamano ya upinzani. Wapinzani wa Maduro wanamiminika mabarabarani takriban kila siku kwa miezi mitatu sasa, kupinga kile wanachokiita kuundwa kwa utawala wa kidikteta. Maandamano hayo yaliosababisha hadi sasa karibu watu 80 kuuwawa, mara nyingi huishia kwenye machafuko na mapambano na askari wa usalama.
Maafisa wa chama tawala cha Kisoshalisti, wametoa mloongo wa matamshi ya kumshambulia mwendesha mashtaka mkuu Luisa Ortega ambaye amekuwa akihudumu pia kama Mwanasheria mkuu, kwamba anachochea machafuko baada ya kujitenga na msimamo wa serikali.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa ya Geneva
Msemaji wa Umoja wa mataifa anayehusika na masuala ya Haki za Binaadamu Rupert Colville, alitoa taarifa mjini Geneva akisema, uamuzi wa mahakama ya Venezuela tarehe 28 mwezi huu wa Juni kuanza mchakato wa muondoa katika wadhifa wake mwanasheria mkuu, kuzizuwia mali zake na kumzuwian pia kusafiri nje ya nchi, ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa sawa na machafuko yanayoendelea nchini humo.
Colville alisema mahakama kuu ya katiba kwa upande mwengine imefuta uteuzi wa Bibi Ortega wa naibu mwanasheria mkuu na kumteuwa mtu mwengine, ikiwa ni kinyume cha sheria.Pia Bibi Ortega amepokonywa baadhi ya majukumu yake na kupewa mtu mwengine.
Tangu mwezi Machi, Mwanasheria mkuu huyo amechukua hatua muhimu kulinda haki za binaadamu, akisisitiza juu ya kutengwa kwa madaraka na maamuzi kulingana na sheria na kuwataka watu waliokamatwa na kuzuiliwa kinyume cha sheria waachiliwe huru.
Rais Maduro anadai kwamba maanadamno ya wapinzani yanayolenga katika kuiangusha serikali yake kwa msaada wa Marekani.
Kwa upande mwengine Umoja wa mataifa umesema umepokea taarifa kwamba askari wa usalama wameyavamia majengo kadhaa ya makaazi, kufanya upekuzi bila ya kibali , kuwaandama wafuasi wa upinzani na kuwakamata watu hovyo. Inasemekana lengo hasa ni kuwazuwia watu wasishiriki katika maandamano ya kuipinga serikali.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman Reuters
Mhariri: Iddi ssesanga