1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Umoja wa Mataifa waonya juu ya mapigano magharibi mwa Darfur

27 Aprili 2024

Umoja wa Mataifa umeonya jana Ijumaa kwamba vikosi vya wanamgambo nchini Sudan vinauzingira mji mkuu pekee ambao hawajauteka wa magharibi mwa Darfur.

Umoja wa Mataifa waonya juu ya mashambulizi magharibi mwa darfur
Mapigano nchini Suda yameendelea kusambaa na kusababisha hali mbaya ya kibinaadamu na wengi kukimbia makazi yaoPicha: Marwan Ali/AP/dpa/picture alliance

Umoja huo umeonya kwamba shambulizi lolote linaweza kuwa na matokeo mabaya kwa wakaazi 800,000 wa jiji hilo na kuongeza kuwa vikosi vinayopigana nchini humo vya SAF na RSF hivi sasa vinajipanga upya.

Ofisi ya umoja huo ya misaada ya kiutu, imesema jana kwamba kuongezeka kwa mapigano karibu na mji El Fasher, Kaskazini mwa Darfur wiki mbili zilizopita yamewafanya watu 40,000 kukimbia, na wengi kujeruhiwa.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema Katibu Mkuu Antonio Guterres kwa mara nyingine alitoa wito kwa pande hizo kujizuia kupigana katika eneo la Kaskazini la Darfur karibu na mji mkuu wake, El Fasher.

Mkuu wa masuala ya siasa wa Umoja huo Rosemary DiCarlo alisema Ijumaa iliyopita kwamba vita hivyo vinavyochochewa na msaada wa silaha kutoka nje na kudumu kwa mwaka mmoja sasa vimesababisha mgogoro mkubwa wa kibinaadamu.