1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Zaidi ya 200 wauwawa kwa mashambulizi ya droni Sudan

13 Machi 2026

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema ameshtushwa na ongezeko la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani nchini Sudan, ambayo yameripotiwa kusabisha vifo vya zaidi ya raia 200 tangu mapema mwezi huu.

Sudan Al-Dabba 2025 | Vertriebene Frauen aus El-Fasher warten auf Lebensmittelhilfe im El-Afadh-Camp
Umoja wa Mataifa umesema mashambulizi ya droni Sudan yamewaangamiza zaidi ya watu 200Picha: Marwan Ali/AP Photo/picture alliance

Taarifa iliyotolewa mjini Geneva inasema pande zinazopigana nchini Sudan zimeongeza matumizi ya teknolojia ya kisasa ya kivita, hasa ndege zisizo na rubani, katika mashambulizi yanayoelekezwa kwenye maeneo ya makazi ya watu.

Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa matumizi hayo yanaongeza madhara kwa raia na yanaharibu miundombinu muhimu.

Katika jimbo la Kordofan Magharibi pekee, ripoti zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 150 waliuawa katika mashambulizi ya droni yaliyolenga masoko, hospitali na magari ya abiria. Tukio baya zaidi liliripotiwa mapema mwezi huu katika mji wa Muglad, ambapo watu wasiopungua 50 walikufa baada ya soko na hospitali kushambuliwa.

Mashambulizi mengine katika masoko mawili yaliyoko kwenye maeneo yanayodhibitiwa na vikosi vya RSF, pia yalisababisha vifo vya raia kadhaa. Aidha, lori lililokuwa limebeba abiria liliripotiwa kupigwa na droni, ambapo takribani watu 50 wakiwemo wanawake na watoto waliuliwa.

Mapigano yaongezeka White Nile

Katika jimbo la White Nile, mapigano yameongezeka kutokana na mashambulizi ya droni katika shule, vituo vya afya na hata mabweni ya wanafunzi. Shambulizi la hivi karibuni katika kijiji cha Shukeiri lilisababisha vifo vya watu wasiopungua 17. Msemaji wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Seif Magango, amesema matumizi yanayoongezeka ya droni yanaathiri vibaya maisha ya raia.

"kuongezeka kwa mashambulizi ya droni tunakushuhudia Sudan kuna madhara makubwa kwa raia na kunashtusha. Ripoti zinaonyesha kuwa zaidi ya raia 200 wameuawa tangu tarehe nne mwezi huu wa Machi maeneo ya Kordofan na pia jimbo la White Nile.”

Katika jimbo la White Nile, mapigano yameongezeka kutokana na mashambulizi ya droni katika shule, vituo vya afya na hata mabweni ya wanafunzi.Picha: Sudanese Ministry of Culture and Information/Xinhua/picture alliance

Vita nchini Sudan vilianza Aprili mwaka 2023 baada ya mvutano kati ya jeshi la taifa na kikosi cha wanamgambo wa RSF kuzuka na kusambaa katika maeneo mengi ya nchi hiyo. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu elfu kadhaa wameuawa huku zaidi ya milioni 11 wakilazimika kuyahama makazi yao.

Mashambulizi yaathiri juhudi za kutoa misaada

Mashirika ya misaada yanasema ongezeko la mashambulizi ya droni pia limeathiri juhudi za kutoa misaada, hasa katika maeneo ya Darfur na Kordofan ambako mahitaji ya chakula na huduma za afya ni makubwa.

Umoja wa Mataifa sasa unazitaka pande zote zinazopigana kuzingatia sheria za kimataifa za vita na kuepuka kuwashambulia raia pamoja na miundombinu ya kiraia. Seif Magongo anasema:

" Ni changamoto kwamba kicha ya kutoa onyo mara kadhaa na pia miito, pande zinazozozana zinaendelea kutumia droni na silaha za kulipuliwa katika zaidi katika maeneo yenye idadi kubwa  ya watu. Tunarudia wito wa Kamishna Mkuu Volker Turk kwa pande husika kuheshimu sheria za vita na kuepuka kushambulia raia na mali za kiraia.”

Kamishna mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker TurkPicha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Wakati mapigano yakiendelea kuenea katika maeneo mapya, viongozi wa kimataifa wanasisitiza haja ya kusitishwa kwa vita hivyo na kuanza mazungumzo ya amani ili kuwaondolea mateso wananchi wa Sudan.

Umoja wa Mataifa umesema ni wakati muafaka sasa wa kumaliza vita hivyo ambavyo vimeharibu maisha na riziki za mamilioni ya watu, huku ukisisitiza kuwa, imetosha sasa, kwa raia wa Sudan kuvumilia mateso.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW