Umoja wa Mataifa umetoa ripoti ya ukiukaji wa haki za binadamu Sudan Kusini
4 Januari 2014Wakati mazungumzo ya amani kati ya Serikali na waasi Sudan kusini yamekwisha anza leo mjini Adis Ababa Ethiopia, mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi, yamekuwa yakiendelea katika maeneo kadhaa yaliyoshikiliwa na waasi.
Kufuatia mapigano hayo huko Sudan Kusini,kamishna mkuu wa umoja wa mataifa anayehusika masuala ya haki za binadamu, Navi Pillay ametoa ripoti inayoainisha ukiukaji wa haki za binadamu iliyoangazia zaidi mauaji ya watu wasio na hatia yanayofanyika kwa kulenga raia kufuatana na kabila na mfululizo wa matukio ya kuwekwa kizuizini kwa watu hao, wengi wao wa maeneo ya mji wa Dinka, baada ya tukio la jaribio la mapinduzi la mwezi Desemba.
Katika ripoti hiyo imefahamika kuwa, askari hao wa pande mbili wakati wa mapigano, walikuwa wakiwaongelesha watu waliowakamata ili kuhakikisha kama wana lafudhi ya kabila lao ama la, na kuwaua wale waliothibitisha kuwa si wa kabila lao. Watu wa Kabila la Dinka waliokamatwa na kusalimika kutoka mikononi mwa askari wa kabila la Nuer, wamekuwa wakitoa shuhuda hizo.
Aidha katika ripoti hiyo iliyotolewa na kitengo cha kusimamia haki za binadamu katika umoja wa Mataifa, kumeainishwa kuwa, wamegundua kaburi la jumla katika eneo la Bentui, na huenda ikawa kuna makaburi mengine ya jumla walau mawili katika mji wa Juba.
Umoja wa Mataifa imeongeza askari wa kulinda amani Sudan Kusini
Idadi ya wanajeshi wa umoja wa mataifa wa kulinda amani inatarajiwa kuongezeka, baada ya kikao cha dharura cha baraza la usalama la umoja wa mataifa kupiga kura wiki iliyopita na kuamua kuongeza askari wengine 5,500, kutoka maeneo mbalimbali duniani, na kufanya kufika idadi ya askari 12,500 waliopelekwa na umoja wa Mataifa kulinda amani huko Sudan Kusini. Zoezi la kupeleka askari hao wa umoja wa mataifa litachukua muda wa wiki tatu.
Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona kuwa, Umoja wa Mataifa imechelewa kuchukua hatua hiyo tangu yalipozuka mapigano hapo Desemba mwaka jana.
Askari wa Umoja wa Mataifa huenda wakadhibiti hali ya mapigano
Wakati askari hao wa umoja wa mataifa wa kulinda amani nchini humo wanapozidi kuwasili, huenda mapigano hayo mapya yaliyozuka yakasimama, lakini huenda swala la mpango wa Riek Machar wa kuendeleza mapigano kwa msimamo wa madai yake na uwezekano wa kupatikana kwa demokrasia ya nchi hiyo na raia wake ukachelewa.
Kwa mujibu wa wachambuzii wa masuala ya kisiasa, mashambulizi kadhaa yaliyofanywa na wanajeshi wanaomuunga mkono Machar katika mji wa Bor na kukubali kwake kupeleka wajumbe wake katika mazungumzo ya amani mjini Adia Ababa, ni shemu ya mkakati wake wa kisiasa katika mvutano wa kuwania madaraka na rais Salva Kirr.
Mwandishi: Diana Kago/IPS
Mhariri: Mohamed Abdul Rahman