1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa una matumaini na mazungumzo ya Libya

9 Novemba 2020

Kiongozi wa mpito wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya, Stephanie Williams ameonyesha matumaini kuelekea katika mazungumzo yanayolenga kufanya maandalizi ya uchaguzi wa nchi hiyo iliyokumbwa na vita. 

Libyen Fortschritte bei Verhandlungen über Waffenstillstand ARCHIV
Picha: picture-alliance/Photoshot/A. Salahuddien

Mazungumzo hayo yanayoongozwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya yanaanza siku ya Jumatatu kwenye mji mkuu wa Tunisia, Tunis na yanafanyika kutokana na utulivu wa miezi kadhaa uliojitokeza nchini Libya, ambayo ilitumbukia katika machafuko mwaka 2011, baada ya kuondolewa madarakani Kanali Muammar Gaddafi.

Mwezi uliopita, pande mbili kuu zinazohasimiana zilisaini makubalino ya kihistoria ya kusitisha mapigano, hatua iliyofungua njia ya kuanza tena kwa shughuli za kuchimba mafuta, ambao ni muhimu kwa uchumi wa Libya. Hali kadhalika hatua iliyopigwa katika juhudi za kuumaliza mkwamo wa kisiasa uliodumu kwa miaka kadhaa.

Akizungumza na waandishi habari mjini Tunis, siku moja kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo, Stephanie Williams amesema hiyo ni fursa ya kipekee na kwamba maendeleo makubwa yamepatikana.

Mazungumzo ya kisiasa ya hivi karibuni ambayo yaliwajumuisha wapatanishi wa kijeshi na kiuchumi, yalikuwa na lengo la kuiunganisha nchi hiyo chini ya utawala mmoja na kufungua njia ya uchaguzi wa kitaifa.

Williams amesema uchaguzi unapaswa kuwa na lengo kuu na kutoa wito wa kuwepo njia sahihi kuelekea kwenye uchaguzi haraka iwezekanavyo.

Hata hivyo, Williams amezungumzia maendeleo yaliyopigwa na hatua zilizochukuliwa ikiwemo mazungumzo ya kijeshi pamoja na kuanza tena kwa safari za ndani za ndege kwenda eneo la kusini mwa nchi hiyo na kuanza tena uchimbaji wa mafuta.

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Stephanie WilliamsPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

"Tayari tunaweza kuona faida, matunda ya kazi ya tume hii ya pamoja ya kijeshi hapa Libya. Tayari tumeona visima vyote vya mafuta viko wazi na kwamba mafuta yanachimbwa na tuko tayari, Shirika la taifa la Mafuta tayari limeripoti kwamba kwa siku mapipa laki nane ya mafuta yanachimbwa," alifafanua Williams.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameuita mchakato huo kama ''hatua ya kinsingi kuelekea kwenye amani na utulivu,'' na kwamba Umoja wa Mataifa umeweka malengo yake, ikiwemo kuanzishwa kwa serikali mpya itakayowashirikisha wawakilishi wakuu wa jamii ya Libya katika mchakato huo na kisha kuandaa uchaguzi wa bunge na urais.

Libya ambayo inadhibitiwa na wanamgambo ambao wanaziunga mkono pande mbili kuu za kisiasa nchini humo, ikiwemo serikali iliyo GNA iliyoko mjini Tripoli na utawala mwingine wa Mashariki unaoongozwa na mbabe wa kivita Jenerali Khalifa Haftar.

Mapambano baina ya vikosi

Vikosi vya Jenerali Haftar vinavyoungwa mkono na Urusi na Umoja wa Falme za Kiarabu, vilianzisha mashambulizi mwezi Aprili mwaka 2019 ili kuuteka mji mkuu, na kusitisha ghafla awamu ya awali ya mazungumzo yaliyokuwa yanaoongozwa na Umoja wa Mataifa.

Lakini vikosi hivyo vilipata upinzani mkali kutoka kwa vikosi vya GNA vinavyoungwa mkono na Uturuki, baada ya kuanzisha mashambulizi yaliyovirudisha nyuma vikosi vya Haftar kwenye mji wa pwani wa Sirte, eneo alikozaliwa Gaddafi.

Mapigano hayo yalisababisha mauaji ya mamia ya watu na maelfu ya watu waliachwa bila maakazi.

Watu 75 wanaoshiriki katika mazungumzo kuhusu nchi hiyo ya Afrika Kaskazini, walichaguliwa na Umoja wa Mataifa ili kuwakilisha muundo wa kisiasa, kijeshi na kijamii wa nchi ya Libya.

(AFP, DW)