Umoja wa Mataifa waonya kitisho cha janga la kiutu Niger
29 Agosti 2023Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema limefanyia marekebisho mipango yake huduma za dharura kwa Niger tangu kufanyika kwa mapinduzi ya kijeshi ya Julai 26 ambayo yaliyomuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum.
Akizungumza na waadhisi wa habari mjini Geneva, Mwakilishi Mkazi wa shirika hilo kwa Niger, Emmanuel Gignac anasema: "Mgogoro wa kisiasa unaoendelea, bila suluhu ya ishara ya suluhisho la wazi, unazua sintofahamu na wasiwasi huku nchi ikiendelea kukumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa makundi ya wenye kujihami kwa silaha, hasa karibu na mpaka wa Mali na Burkina Faso".
UNHCR yarekodi zaidi ya wakimbizi 20,000 kwa Julai
Onyo hilo linatolewa katika kipindi ambacho zaidi ya watu 20,000 kwa rekodi za mwezi uliopita wameyakimbia makazi yao. Mwakilishi huyo wa UNHCR kadhalika ameonya kuwa "hali hiyo imeongeza hatari za kusalama kwa wakimbizi, wanaotafuta hifadhi na wenyeji wao".
Kimsingi UNHCR imeshuhudia ongezeko la asilimia 50 za kile kinachoitwa matukio ya kiusalama, ikiwa ni pamoja na utekaji nyara, unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji mwingine, ikiwa ni takribani siku tano tu, baada ya mapinduzi ya kijeshi.
Kupanda kwa bei ya vyakula kunakotokana na vikwazo vya ECOWAS
Mwakilishi Gignac alidokeza kuwa kufungwa kwa mipaka na vikwazo vilivyowekwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) kwa watawala hao wapya wa kijeshi kumesababisha kupanda kwa bei za vyakula na bidhaa.
Vikwazo vinaweza kuchochea kutofika kwa misaada ya kiutu kwa wenye kuhitaji, hali ambayo inaweza kusababisha baa la njaa.
Walio hatarini zaidi ni raia takribani 350,000 wa Niger ambao tayari wamekuwa wakimbizi wa ndani kwenye taifa lao, ikiwa pia kuna idadi sawa na hiyo ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi kutoka nchi jirani.
Soma zaidi:Utawala wa Kijeshi Niger wampa balozi wa Ufaransa saa 48 kuondoka nchini humo
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kuhudumiwa wakimbizi UNHCR limesema hadi wakati huu hakuna ripoti za harakati kubwa za watu kutoka Niger kukimbilia mataifa jirani lakini si jambo ambalo haliwezi kutokea pale ambapo kunaweza kutokea uvamizi wa kijeshi au jambo lingine lolote litakalozua hofu kwa raia.
Chanzo: AFP