Umoja wa Mataifa unakabiliwa na mzozo wa fedha
9 Oktoba 2019Akizungumza na waandishi habari msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema kuwa Guterres ameziandikia barua nchi zote wanachama akisema umoja huo uko katika hatari ya kuimaliza akiba yake ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.
Guterres amezitaja nchi hizo kuwa ni pamoja na Marekani, ambayo ndiyo mchangiaji mkubwa wa Umoja wa Mataifa. Amesema iwapo fedha hizo hazitatolewa, umoja huo utashindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wake na wanaotoa huduma. Dujarric amesema hadi jana, nchi 129 zimelipa Dola bilioni 1.9 kama ada zao kwa mwaka 2019.
Syria ya mwisho kuchanga
''Mwanachama aliyelipa pesa zote hivi karibuni ni Syria ambayo ndiyo inafikisha idadi ya nchi 129. Hadi sasa nchi wanachama wamelipa Dola bilioni 1.99 kuelekea katika tathmini ya bajeti ya kawaida ya mwaka 2019. Kiasi ambacho bado hakijalipwa mwaka huu ni Dola bilioni 1.3,'' alifafanua Dujarric.
Dujarric amesema hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Septemba, nchi wanachama zilikuwa zimelipa asilimia 70 ya fedha jumla ya bajeti ikilinganishwa na asilimia 78 katika kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita. Mbali na Marekani nchi nyingine ambazo hazijalipa ada ya mwaka ni pamoja na Brazil, Iran, Israel, Mexico, Korea Kusini, Saudi Arabia, Uruguay, Venezuela na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Mzunguko wa fedha ni tatizo
Guterres amesisitiza kwamba mzunguko wa fedha ni tatizo ambalo limekuwa likijirudia na Umoja wa Mataifa hauna budi kwa sasa kuhakikisha matumizi yake yanaendana na kiwango cha fedha kilichopo, hali inayodhoofisha mamlaka na majukumu yake kwa watu wanaowahudumia.
Dujarric amesema kwa sababu umoja huo unaweza ukakosa fedha za kuwalipa wafanyakazi wake ifikapo mwishoni mwa wezi Novemba, Guterres ameomba hatua za haraka zichukuliwe ikiwemo kupunguza safari za kikazi, kuahirisha manunuzi ya bidhaa na huduma, kusitisha shughuli zilizopangwa nje ya muda rasmi wa kazi na kwamba mikutano inaweza kuahirishwa au huduma zikabadilishwa.
Hata hivyo, kulingana na kalenda ya bajeti ya serikali ya Marekani, nchi hiyo kwa kawaida huwa inalipa mchango wake mwezi Oktoba. Umoja wa Mataifa umesema unaidai Marekani Dola milioni 674 kwa mwaka 2019 na Dola milioni 381 kwa ajili ya bajeti za kawaida zilizopita. Marekani pia haijatoa malipo ya bajeti tofauti kwa ajili ya shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.
(AP, AFP)