Umoja wa Mataifa waanzisha masomo ya bure kuhusu mazingira
4 Desemba 2014Kozi hiyo iliyopewa jina la "Majanga na Mifumo ya Mazingira: Uwezo wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi" inaanza rasmi tarehe 12 Januari 2015 itakuwa inafundishwa moja kwa moja kupitia mtandaoni, ambapo wakufunzi kutoka Ujerumani, Misri, Uswisi na Austria watatoa mihadhara ya kitaaluma na vitendo juu ya mabadiliko ya tabia nchi, upunguzaji wa athari za mabadiliko hayo na uhifadhi wa mazingira.
Walengwa wa kozi hii ya mtandaoni ni takribani kila mtu ambaye anataka kujielimisha juu ya udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabia nchi, wakiwemo wanafunzi, wafanyakazi, wasimamizi wa miradi, viongozi na hata raia wa kawaida wanaojali hatima ya jamii zao. Washiriki watakaokamilisha mafunzo hayo watapatiwa cheti.
Mratibu wa mafunzo hayo kwenye Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, Mahesh Pradhan, alisema tayari wameanza kupokea maombi kutoka pande mbalimbali duniani. "Kwa kuanzisha kozi hii ya mtandaoni, sio tu tunatoa taaluma inayohitajika kwenye suala la uhusiano kati ya majanga ya kimaumbile na mabadiliko ya tabia nchi bila malipo, bali pia tunawajumuisha walimwengu wote bila kujali mipaka ya kiumri na kimataifa." Anasema Pradhan.
Chuo Kikuu cha Taaluma za Sayansi cha Cologne, ambacho ni sehemu ya mpango huu, ni miongoni mwa vyuo vikongwe na vyenye heshima kubwa sana barani Ulaya. Kikiwa na jumla na wanafunzi 23,000 wanaosomea kozi zaidi ya 80 zinazofundishwa na kiasi cha maprofesa 420, chuo hicho ni mwanachama wa Umoja wa Vyuo Vikuu Barani Ulaya, EUA.
Rais wa chuo hicho, Christoph Seeßelberg, anasema miongoni mwa sababu za chuo chake kujihusisha moja kwa moja wa kozi hii ni kutaka kutumia utaalamu wake kuwasaidia wanaadamu kujikinga na athari za tabianchi, sambamba na kuwaokoa viumbe walio hatarini kutoweka kutokana na athari hizo.
Kwa ujumla, kozi hii imegawiwa kwenye viwango viwili: kiwango kilichopewa jina la "eneo la uongozi" ambacho kina vipengele sita vya masomo yaliyolengwa kuwagusa watu wote na wenye historia yoyote ya kitaaluma. Lengo kuu la kiwango hiki cha kozi ni kuwapatia washiriki mtazamo wa jumla wa uwiano uliopo kati ya majanga ya kimaumbile na mabadiliko ya tabia nchi.
Kiwango cha pili ni kile kilichopewa jina la "eneo la wataalamu", ambacho kina vipengele 15 vinavyoingia kwa undani kwenye masuala ya nyenzo za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na namna jamii zinavyoweza kutangamana na hali halisi ilivyo.
Katika viwango vyote viwili, washiriki wanapata fursa ya kuchangiana mawazo na mtandao wa wanafunzi duniani kote, wakiwa wanaunganishwa na fungamano la kupunguza majanga ya kimazingira duniani, PEDRR.
Kujisajili kwenye kozi hii mtu anapaswa kuingia kwenye kiungo hiki: https://iversity.org/en/courses/disasters-and-ecosystems-resilience-in-a-changing-climate.
Mwandishi: Mohammed Khelef
Chanzo: UNEP
Mhariri: Iddi Ssessanga