Umoja wa Mataifa waanzisha ujumbe wa kisiasa kusaidia Sudan
4 Juni 2020Rasimu ya Umoja wa Mataifa kuanzisha Ujumbe wa kuisaidia Sudan katika mchakato wake wa mpito wa kisiasa (UNITAMS) ilitayarishwa na Ujerumani pamoja na Uingereza. Kulingana na rasimu hiyo ambayo shirika la habari la AFP imeiona, Ujumbe huo unapaswa kudumu kwa muda wa mwaka mmoja. Rasimu hiyo inamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kumteua kwa haraka mjumbe atakayeuongoza ujumbe huo.
Baada ya aliyekuwa rais wa muda mrefu Omar al-Bashir kuangushwa mnamo Aprili mwaka 2019, na pia baada ya miezi kadhaa ya maandamano ya kupigania demokrasia ambayo ilikuwa ikikandamizwa, Sudan ilianzisha mchakato wa mpito wa kisiasa.
UNAMID kuhudumu hadi Disemba 31
Mnamo Agosti mwaka uliopita, baraza la mpito liliundwa likiwajumuisha maafisa wa kijeshi pamoja na raia kuongoza mchakato wa mpito kwa kipindi cha miaka mitatu. Uingereza na Ujerumani zilitayarisha rasimu ya kuanzisha tena operesheni ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika (UNAMID) katika eneo la Darfur, hadi Disemba 31.
Rasimu hiyo ambayo AFP imeiona pia inataka kikosi kilichoko sasa eneo hilo chenye wanajeshi 8,000 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kuendelea kuhudumu.
Maswali kuhusu muda wa UNAMID
Hata hivyo, mnamo mwezi Machi, Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Afrika ulipendekeza kuwa ujumbe wa UNAMID ubadilishwe na nafasi yake ichukuliwe na ujumbe wa kisiasa ifikapo mwezi Oktoba, kando na kutaka walinda amani waondolewe taratibu.
China, Urusi na nchi kadhaa za Afrika ziliunga mkono mpango huo, lakini nchi za Ulaya pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali yalielezea hofu kwamba raia wataachwa bila ulinzi endapo ghasia zitaongezeka.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, machafuko ya Darfur kati ya vikosi vya Sudan pamoja na waasi kutoka makabila madogo yanayodai kutengwa na serikali kuu, yamesababisha takriban vifo vya watu 300,000 na zaidi ya watu milioni 2.5 wamelazimishwa kuyakimbia makaazi yao tangu mwaka 2003.
Chanzo: AFPE
Mwandishi: John Juma
Mhariri: Josephat Charo