1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wafunga ofisi yake Sri Lanka

Josephat Nyiro Charo9 Julai 2010

Umoja wa Mataifa pia umemuondoa mjumbe wake kufuatia maandamano ya kupinga kazi inayofanywa na jopo la umoja huo, linalochunguza visa vya ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na wanajeshi wa serikali wakati wa vita

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture-alliance / dpa

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amechukua hatua kali dhidi ya maandamano yanayoongozwa na waziri wa ujenzi wa Sri Lanka, Wimal Weerawansa, nje ya ofisi ya umoja huo mjini Colombo kwa kuifunga ofisi ya umoja huo na kumuamuru mjumbe wake mkuu nchini humo, Neil Buhne, arejee makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mjini New York, Marekan kwa mashauriano.

Ban Ki Moon amesema haikubaliki kwamba maafisa wa Sri Lanka wameshindwa kuzuia maandamano hayo yaliyoitatiza kazi ya wafanyakazi wa umoja huo mjini Colombo, ambao walilazimika kufunga ofisi yao Jumatano wiki hii. Ameitaka serikali ya Sri Lanka itimize ahadi na majukumu yake kwa Umoja wa Mataifa kama nchi mwenyeji, ili chombo hicho cha kimataifa kiweze kuendelea na kazi yake muhimu ya kuwasaidia raia wa nchi hiyo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, amesema "Tumekuwa tukiitegemea serikali ya Sri Lanka kuheshimu ahadi zake kama nchi mwenyeji katika makubaliano yake na Umoja wa Mataifa, kuwaruhusu wafanyakazi kufanya kazi yao bila vikwazo. Lakini tulichokishuhudia tangu siku ya Jumanne ni kutatizwa kwa maafisa wetu kiasi cha kutoweza kuendelea na kazi yao."

Waziri wa nyumba wa Sri Lanka Wimal WeerawansaPicha: AP

Maandamano ya mjini Colombo yamekuwa yakiongozwa na waziri wa ujenzi, Wimal Weerawansa, mwanasiasa wa kizalendo ambaye ni mshirika mkubwa wa rais Mahinda Rajapaksa. Hapo jana Weerawansa alianza mgomo wa kufunga, na ameapa kuendelea na saumu yake mbele ya ofisi ya Umoja wa Mataifa licha ya ofisi hiyo kufungwa.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ilifunguliwa kuwaruhusu baadhi ya wafanyakazi wake hapo jana baada ya maandamano kukumbwa na machafuko wakati waandamanaji walipokabiliana na polisi waliokuwa wakijaribu kuwasindikiza wafanyakazi wa umoja huo kutoka ofisi hiyo.

Waandamanaji wanaiunga mkono serikali katika dai lake la kuutaka Umoja wa Mataifa ulivunjilie mbali jopo lililoteuliwa na Ban Ki Moon mwezi uliopita kuchunguza na kumshauri ikiwa uhalifu wa kivita ulifanyika mwishoni mwa vita vya miaka 25 kati ya waasi wa Tamil Tigers na vikosi vya serikali. Wanajeshi wa serikali waliwachakaza waasi hao mnamo mwezi Mei mwaka jana 2009.

Waandanaji wa Sri Lankan wakiwa wamebeba benderaPicha: AP

Sri Lanka inaliona jopo hilo kama chombo kinachouhujumu uhuru wake na unafiki wa serikali za mataifa ya magharibi kuendeleza undumilakuwili katika vita dhidi ya ugaidi. Sri Lanka pia ina wasiwasi kwamba jopo hilo litafungulia mlango uchunguzi kamili.

Ban Ki Moon anasema jopo hilo ni la kuisadia Sri Lanka katika juhudi za kuleta maridhiano, baada ya maelfu ya Watamil kuuwawa katika miezi ya mwisho ya vita nchini humo.

Makundi ya haki za binadamu yametaka kufanyike uchunguzi wa kimataifa wa visa vya ukiukaji wa haki za binadamu kufuatia mauaji ya maelfu ya raia na Sri Lanka inakabiliwa na shinikzo kubwa kutokana na kumbukumbu yake mbaya ya haki za binadamu. Serikali inakanusha kwamba wanajeshi wake walifanya uhalifu wakati wa vita.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE

Mhariri: Aboubakar Liongo