1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wagawanyika kuhusu mauaji

29 Novemba 2018

Mashirika matano ya kimataifa ya habari yameonyesha kwamba maafisa wa Umoja wa Mataifa waliokuwa wanachunguza mauaji ya wataalam wawili Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo walikuwa njia panda kuhusu ukweli na uongo.

Zaida Catalan
Picha: Getty Images/AFP/B. Ericson

Mashirika hayo yanasema hayakujua iwapo yatafute ukweli kuhusu mauaji hayo au yairidhishe serikali ya nchi hiyo.

Uchunguzi huo uliofanywa kwa awamu nne na ambao awamu ya kwanza ilitolewa Jumatano, unajikita katika kuchunguza mauaji ya raia wa Marekani Michael Sharp na raia wa Sweden Zaida Catalan mnamo Machi 2017. Walikuwa wanachunguza madai ya makaburi ya halaiki katika jimbo la kati lenye vita la Kasai, walipotekwa na kuuwawa, jambo lililoupelekea Umoja wa Mataifa kuanzisha uchunguzi wa aliyehusika.

Uchunguzi wa pamoja ulifanywa na mashirika kadhaa

Miezi mitano baadae, kikao cha Umoja wa Mataifa kiliamua kwamba watu hao wawili waliuwawa baada ya kuvamiwa ghafla na kundi la wanamgambo, huku wakikataa kuondoa uwezekano wa serikali kuhusika katika mauaji hayo.

Jimbo la Kasai limekumbwa na mapigano kwa muda mrefuPicha: Reuters/Staff

Lakini uchunguzi wa pamoja wa shirika la Foreign Policy FP na Radio ya Kimataifa ya Ufaransa RFI, gazeti la Le Monde, televisheni ya Sweden ya Sveriges na gazeti la Ujerumani na Suddeutsche Zeitung, umeonyesha kwamba Umoja wa Mataifa ulificha ushahidi ulioeleza kwamba huenda mamlaka za Congo zilihusika katika mauaji hayo.

Uchunguzi wao ulitokana na kuangazia maelfu ya stakabadhi za ndani za Umoja wa Mataifa na mahojiano mengi na wahusika wakuu. Uchunguzi huo umeonyesha kuwa haiko wazi kutokana na stakabadhi hizo ni kwanini uongozi wa Congo ulitaka Sharp na Catalan wauwawe. Lakini unasema kuwa uwezekano mmoja ni kwamba walitaka kuficha uwezekano wa wawili hao kufichua unyama wa serikali katika mkoa wa Kasai.

Wachunguzi walipewa taarifa za uongo

Serikali ya Congo imesema wataalam hao waliuwawa na wanachama wa kundi la waasi la Kamwina Nsapu ambalo lilikuwa likipigana na serikali mkoani kasai tangu Agosti 2016.

Umoja wa Mataifa ulikumbwa na changamoto nyingi katika uchunguzi wake CongoPicha: DW/Flávio Forner

Wachunguzi katika jopo huru la Umoja wa Mataifa waliokuwa wanafanya kazi na kundi la kwanza la Umoja huo, wanasema walipewa taarifa za uongo na serikali ya Congo ambayo ilihitilafiana na ushahidi na ikafanya juhudi ndogo kuwasaidia kupata mahojiano na mashahidi wakuu.

Julai mwaka 2017, mwezi mmoja kabla kuchapishwa kwa matokeo ya jopo hilo, wataalam wa Umoja wa Mataifa waliwasilisha ripoti ya siri katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo hawakuuondoa uwezekano wa kuhusika kwa maafisa wa usalama katika mauaji hayo.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW