UM wahofia kusambaratishwa mkataba wa amani Colombia
24 Novemba 2021Akizungumza baada ya kutembelea kambi inayowahifadhi waasi wa zamani wa kundi la FARC, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisema ingawa serikali imekuwa ikichukuwa hatua kadhaa kuhakikisha mkataba huo wa amani unafanikiwa, bado kunahitajika msaada zaidi wa serikali kuhakikisha maisha ya wapiganaji wa zamani wa waasi hayaharibiki.
Katika kambi hiyo kwenye jimbo la Antioquia, Guterres aliyeambatana na Rais Ivan Duque wa Colombia alishuhudia hali halisi wanayokabiliana nayo wapiganaji hao wa zamani, na akaelezea kusikitishwa kwake na taarifa kwamba wale aliowaita maadui wa amani, wanawaandama walioamua kuutekeleza mkataba wa mwaka 2016 kwa vitisho, utekaji na hata mauaji.
"Nimepatwa na wasiwasi niliposikia maeneo kadhaa bado yanakabiliwa na athari za ukosefu wa usalama. Matendo ya makundi haramu yenye silaha na mauaji ya viongozi, wapiganaji wa zamani na watetezi wa haki za binaadamu yanayapoteza matumaini ya watu. Amani ya Colombia inahitajia kwanza amani ya kwenye mikoa. Na nawanasihini mutumie fursa hii ya kihistoria kuigeuza hamu ya kuwa na amani kuwa ukweli," alisema Guterres.
Marekani yaiondowa FARC kwenye ugaidi
Wakati huo huo, utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani umeliarifu bunge la nchi hiyo kwamba unaliondowa kundi la FARC kwenye orodha ya makundi ya kigaidi, miaka mitano baada ya mkataba huo wa amani kutiwa saini, kwa mujibu wa afisa mmoja wa Congress ambaye hakutaka kutajwa jina.
Msemaji wa Wizara ya Nje ya Marekani, Ned Price, amethibitisha kwamba serikali imeliarifu bunge hilo juu ya hatua inayotaka kuchukuwa kuhusiana na kundi la FARC, ingawa hakufafanuwa hatua yenyewe.
Uamuzi wa kuiondowa FARC kwenye orodha ya magaidi inayawezesha sasa makampuni ya Kimarekani kuwaajiri waliowahi kuwa wapiganaji wa kundi hilo kwenye shughuli zake, zikiwemo za kusaidia uteguwaji wa mabomu ya ardhini yaliyotegwa na kundi hilo katika siku zao za mapambano dhidi ya serikali kuu mjini Bogota.
Kundi la FARC lilisaini makubaliano ya amani na serikali mwaka 2016 yaliyopelekea wapiganaji wake 13,000 kuweka silaha zao chini na kujiunga kwenye makambi ya kuwaandaa kurudi katika maisha ya kawaida.
Makubaliano hayo ndiyo yaliyomaliza mzozo huo ambao hadi hapo ulishasabisha vifo vya watu 260,000 na kuwafanya mamilioni kuwa wakimbizi.
Kwa sasa, FARC ni chama cha kisiasa chenye viti vya uhakika kwenye bunge la Colombia.