Umoja wa Mataifa waidhinisha upelekaji misaada Syria
15 Julai 2014Hata hivyo Syria imetoa onyo kwa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa inaiangalia hatua hiyo ya kupeleka misaada kuwa ni kuingilia ndani ya mipaka yake.
"Ridhaa ya maafisa wa Syria haitakuwa muhimu tena," balozi wa Luxembourg katika Umoja wa Mataifa Sylvie Lucas amewaambia wajumbe 15 wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kura kuhusu azimio hilo, ambalo liliandaliwa na Luxembourg, Australia na Jordan.
Azimio hilo ambalo lilipitishwa kwa kauli moja litakalodumu kwa muda wa siku 180 na mfumo wa uchunguzi kwa ajili ya upakiaji wa shehena ya misaada katika milolongo ya magari katika nchi jirani, ambazo zitaiarifu tu Syria kuhusu aina ya msaada huo wa kiutu katika shehena hizo.
Watu milioni kadha wanahitaji msaada
Umoja wa mataifa umesema kuwa kiasi ya watu milioni 10.8 nchini Syria wanahitaji msaada, ambapo watu milioni 4.7 wako katika maeneo ambayo ni vigumu kufikiwa.
Kiasi ya watu 150,000 wameuwawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria , ambavyo viko katika mwaka wa nne hivi sasa.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power ameishutumu serikali ya Syria kwa kutumia kuzuwia misaada , kama "silaha nyingine katika hazina ya silaha zake za maangamizi na za kikatili dhidi ya maeneo yanayoshikiliwa na upinzani."
Serikali ya Syria imelionya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita kuwa kupeleka misaada kupitia katika mipaka kwenda katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi bila ridhaa itakuwa sawa na shambulio dhidi ya nchi hiyo.
Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Ja'afari ameliambia baraza hilo baada ya kura iliyopigwa jana kuwa serikali ya Syria inategemea jukumu lisilo elemea upande wowote, linalotekelezeka na la uwajibiukaji kutoka kwa Umoja wa Mataifa katika kushughulikia hali ya kiutu nchini Syria, hususan inapokuja suala la kuheshimu mipaka ya Syria.
Azimio hilo pia linaidhinisha upelekaji wa misaada kuvuka mipaka ya maeneo yenye mzozo.
Bashar al-Assad kuapishwa Alhamis
Wakati huo huo rais Bashar al-Assad katika sherehe za kuapishwa siku ya Alhamis anatarajia kujiweka katika hali ya kuwa "mshindi " wakati akijaribu kuwavutia Wasyria ambao wamechoshwa na vita pamoja na wale ambao wanahofia kusonga mbele kwa makundi ya kijihadi.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema Assad ambaye amerejeshwa madarakani katika uchaguzi wa hapo Juni 3 ambao umeshutumiwa kuwa ni kichekesho na upinzani, pia atajaribu kuyashawishi mataifa ya magharibi kuwa utawala wake ni ngome dhidi ya kundi la Waislamu wenye imani kali la Taifa la Kiislamu IS, ambalo linaendesha mapambano ya kigaidi nchini Syria na Iraq.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman