Umoja wa Mataifa waifutia Iran mwaliko
21 Januari 2014Uamuzi huo wa Ban Ki-moon ulifikiwa baada ya Iran kutupilia mbali mashariti yaliyokuwa yakiambatanishwa na mwaliko huo. Msemaji wake Martin Nesirky amesema Ban Ki-moon ameubatilisha mwaliko kwa Iran, baada ya nchi hiyo kukiuka yale waliyokubaliana.
''Katibu mkuu amehuzunishwa sana na tangazo lililotolewa na Iran, ambalo ni kinyume kabisa na ahadi iliyokuwa imetolewa, na anaendelea kuitolea wito nchi hiyo kuunga mkono maazimio ya mkutano wa Geneva.'' Amesema Nesirky.
Mwaliko huo uliotolewa ghafla juzi jioni haukudumu hata kwa saa 24, na ulikuwa umesababisha mtafaruku mkubwa, huku upinzani nchini Syria ukitishia kujitenga kabisa na mkutano wa kesho iwapo Iran ambayo ni mshirika mkubwa wa rais Bashar al-Assad ingeshiriki kwenye meza ya mazungumzo.
Iran 'ilikiuka' ahadi zake
Umoja wa Mataifa umesisitiza kwamba waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Javad Zarif alikuwa amemhakikishia Ban Ki-moon kwamba anaelewa vilivyo, na anaunga mkono lengo la mazungumzo ya amani ambalo ni kuunda serikali ya mpito.
Lakini kabla ya kubatilishwa kwa mwaliko huo kwa Iran, balozi wa nchi hiyo kwenye Umoja wa Mataifa Mohammad Khazaee alikariri msimamo wa serikali yake, kwamba ikiwa kushiriki kwake katika mazungumzo kunafunganishwa na masharti ya kukubali maazimio ya mkutano wa kwanza wa Geneva, basi haitakwenda katika mkutano wa pili.Umoja wa Mataifa umesema katibu mkuu Ban alifanya mashauriano na Marekani na Urusi kabla ya kufuta mwaliko kwa Iran.
Marekani imesema inazo taarifa kutoka ndani ya serikali ya mjini Damascus, kwamba serikali hiyo inataka suluhisho la amani kwa mgogoro unaoendelea nchini humo.
Ingawa mkutano wa Montreux ambao pia umepachikwa jina la Geneva II unaanza kesho, wajumbe wa serikali ya Syria na wa upinzani wataanza kuzungumza Ijumaa. Bado vipo vizingiti vikubwa kwa mazungumzo hayo, ambavyo vimedhihirishwa na mpasuko wa ndani kwa upande wa waasi, msimamo mkali wa rais Bashar al-Assad, na kuendelea kwa ghasia ambazo zinavuka mpaka na kuingia katika nchi jirani.
Mkusanyiko wa kiitifaki
Urusi ambayo ni mshirika wa serikali ya Syria na mmoja wa waandaaji wa mkutano wa Geneva, imesema litakuwa kosa kubwa kutoishirikisha Iran katika mkutano huo. Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Moscow muda mfupi uliopita, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema bila Iran mkutano wa kesho hautakuwa na chochote zaidi ya utaratibu wa kiitifaki. Iran nayo imesema ina mashaka juu ya mafanikio ya mkutano huo.
Muungano mkuu wa upinzani dhidi ya serikali ya rais Bashar al-Assad umesema utakwenda kwenye mkutano huo utakaofanyika katika mji wa Montreux, lakini kundi jingine kubwa lijulikanalo kama Baraza la Kiataifa la Syria limejitenga na mazungumzo hayo, likishikilia msimamo wake wa kutoshiriki mazungumzo yoyote hadi pale rais Assad atakapokuwa ameondoka madarakani.
Kwa mujibu wa takwimu za shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria ambalo lina makao yake nchini Uingereza, watu takribani 130,000 wamekwishauawa katika vita wenyewe kwa wenyewe vya Syria ambavyo vilizuka mwaka 2011.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae/afpe
Mhariri: Ssessanga, Iddi