1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Umoja wa Mataifa waikosoa Myanmar kuhusu demokrasia

Josephat Charo
3 Agosti 2021

Umoja wa Mataifa umeukosoa uamuzi wa utawala wa Myanmar kuchelewesha uchaguzi na kurefusha utawala wa hali ya dharura ukisema ni hatua inayokwenda kinyume na miito ya kimataifa kutaka nchi hiyo irejeshe demokrasia.

USA Sprecher des UN-Generalsekretärs Stéphane Dujarric in New York
Picha: Imago/ZUMA Press/M. Brochstein

Baada ya mtawala wa kijeshi wa Myanmar Min Aung Hlang kujitangaza kuwa waziri mkuu siku ya Jumapili na kusema ataiongoza nchi wakati wa kipindi cha utawala wa hali ya dharura kilichorefushwa hadi uchaguzi utakapofanyika katika kipindi cha takriban miaka miwili, Stephane Dujarric, msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Umoja wa Mataifa, amesema uamuzi huo ni kinyume kabisa na yale ambayo wamekuwa wakiyataka kwamba nchi hiyo irejee katika utawala wa kidemokrasia, wafungwa wote wa kisiasa waachiwe huru, machafuko yasitishwe na ukandamizaji ukome.

"Hautupeleki katika njia sahihi. Unatupeleka mbali kabisa na kile ambacho tumekuwa tukikitaka, ambacho pia nchi wanachama zimekuwa zikikidai, ambacho ni kurejea katika utawala wa kidemokrasia."

Dujarric amesema miezi sita tangu mapinduzi ya kijeshi ya Februari mosi, maelfu ya watu bado wanazuiliwa na hali inazidi kufanywa kuwa mbaya na janga la virusi vya corona. Ameongeza kusema hatua ya pamoja kushughulikia mzozo wa Myanmar inabaki kuwa na umuhimu mkubwa. 

Marekani imeukosoa mpango wa uchaguzi wa Myanmar ikisema utawala wa kijeshi unajaribu kuvuta muda kwa manufaa yake huku waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken akijiandaa kuzihimiza nchi wanachama wa jumuiya ya mataifa ya kusini mashariki mwa Asia ASEAN kumteua mjumbe maalumu kwa ajili ya Myanmar.

Erywan bin Pehin Yusof, wa nne kutoka kuliaPicha: picture-alliance/Zuma Press/C. Subprasom

Mjumbe maalumu kwa mzozo wa Myanmar ateuliwa

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa jumuiya hiyo wamemteua waziri wa pili wa mambo ya nje wa Brunei Erywan bin Pehin Yusof kuwa mjumbe maalumu kwa ajili ya Myanmar, katika uamuzi ulioafikiwa jana Jumatatu. Kwa sasa bado wanasubiri ridhaa kutoka kwa viongozi wa kijeshi wa Myanmar kabla kumtangaza rasmi.

Waziri wa mambo ya nje wa Indonesia Retno Marsudi ameihimiza Myanmar iridhie uteuzi wa mjumbe maalumu wa jumuiya ya ASEAN. "Nawasilisha kwa uwazi kabisa kuwa jumuiya ya ASEAN haijapiga hatua kubwa ya maana katika utekelezaji wa mpango wa vipengee vitano kuhusu Myanmar. Indonesia inatumai Myanmar itaridhia mara moja uteuzi wa mjumbe maalumu."

Mtawala wa kijeshi wa Myanmar Min Aung Hlaing alihudhuria mkutano wa ASEAN kuhusu mzozo wa nchi yake mnamo Aprili mjini Jakarta, Indonesia, uliomalizika na taarifa ya pamoja iliyotaka machafuko yakome mara moja na kuteuliwe mjumbe maalumu wa jumuiya hiyo kwa ajili ya Myanmar ambaye jukumu lake ni kutafuta njia za kufikisha mwisho machafuko na kuhimiza mdahalo kati ya utawala wa kijeshi na wapinzani wake. Lakini baadaye kiongozi huyo alijitenga kabisa na taarifa hiyo, hakuna mjumbe aliyeteuliwa na zaidi ya watu 900 wanaripotiwa wameuliwa katika kipindi cha miezi sita ya ukandamizaji.

(ap, afpe)