Umoja wa Mataifa waondoa vikwazo vya silaha Afrika ya Kati
28 Julai 2023Azimio la kuondoa vikwazo vyote vya silaha kwa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati lilipitishwa kwa kura 13. Urusi na China hazikushiriki katika kura hiyo.
Hata hivyo Baraza la Usalama limeamua kuendelea kuweka vikwazo vya silaha kwa makundi ya mamluki na wapiganaji wenye silaha nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sylvie Baïpo-Temon, ameliambia baraza hilo baada ya kumalizika upigaji kura kwamba marufuku ya silaha kwa nchi yake iliyowekwa mwaka 2013, ilipaswa kuondolewa kwa ukamilifu na sio nusu nusu. Ameliiita azimio hilo kuwa ni la kibaguzi akidokeza kwamba hiyo ni kazi ya nchi zenye nguvu kutoka kambi ya Magharibi.
Azimio lililopitishwa jana Alhamisi halikutaja waziwazi kundi la mamluki la Wagner la nchini Urusi lakini linalaani shughuli za uhalifu wa kuvuuka mipaka, usafirishaji haramu wa silaha ndogo ndogo ambazo zinatishia amani na usalama huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.