1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

UN yaionya Ulaya dhidi ya kusitisha msaada Afghanistan

25 Januari 2023

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed amezionya nchi wanachama za Umoja wa Ulaya kuhusu kusitisha msaada wa kiutu nchini Afghanistan, licha ya utawala wa Taliban kukandamiza haki za wanawake.

USA | Amina J. Mohammed - Vereinte Nationen
Picha: Luiz Rampelotto/ZUMA Wire/IMAGO

Akizungumza jana Jumanne na waandishi habari mjini Brussels, Amina amesema serikali zinahitaji kuwaeleza walipa kodi kwa nini wanaendelea kutoa fedha katika nchi ambayo inawabagua wanawake kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, amesema ukweli mchungu ni kwamba wanawake na watoto nchini Afghanistan watakufa bila ya kupata msaada kutoka nje ya nchi.

Baadhi ya Waafghani hawana chakula cha kutosha

Akizungumzia umuhimu wa msaada wa kiutu, Amina amesema Afghanistan inashuhudia viwango vya joto vikishuka hadi nyuzi 30 chini ya sifuri katika kipimo cha Celsius na baadhi ya watu hawana chakula cha kutosha. Lengo la jumuiya ya kimataifa linapaswa kuwashinikiza wapiganaji wa Taliban kwenye maeneo mengine kubatilisha maamuzi ya kibaguzi dhidi ya wanawake.

Amefafanua kuwa marufuku ya ajira na mafunzo kwa wanawake inawaathiri pia wafanyakazi wa kike wa mashirika ya kutoa misaada. ''Hilo halikubaliki kwangu na nitapambana hadi tutakapohakikisha wanajumuishwa, kwa sababu ikiwa tutawaacha wanawake wa Afghanistan, ni wanawake wangapi wengine ambao tutawakatia tamaa pindi hali inapokuwa ngumu?'', alisisitiza Naibu huyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Wanafunzi wa kike wa Afghanistan wakienda shule kabla Taliban haijapiga marufuku elimu kwa wasichana na wanawakePicha: AFP

Nchi wanachama za Umoja wa Ulaya kwa sasa zinatafakari iwapo kuendelea kutoa msaada wa kiutu kwa Afghanistan ni suala ambalo bado linawezekana kulingana na mazingira ya sasa. Siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock alipendekeza msimamo mkali wakati wa mkutano na mawaziri wenzake wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Baerbock alisema ikiwa wanawake hawawezi tena kufanya kazi katika mashirika ya kimataifa, basi msaada hautowafikia tena. Amebainisha kuwa wao kama jumuia ya kimataifa, hawawezi kuwa chini ya Taliban kutokana na kuwapiga marufuku wanawake kufanya kazi.

Guterres: Taliban ibatilishe marufuku ya elimu kwa wasichana

Wakati huo huo, katika kuadhimisha Siku ya Elimu Duniani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameutaka utawala wa Taliban kubatilisha marufuku inayowakataza wanawake na wasichana kupata elimu ya sekondari na elimu ya juu. Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO mwaka huu limeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Elimu maalum kwa ajili ya wasichana na wanawake wa Afghanistan. Siku hiyo huadhimishwa kila Januari 24.

Wanawake wa Afghanistan wamekuwa wakitetea haki zao katika njia tofauti ikiwemo maandamano ya umma, ambayo kwa kawaida hukandamizwa na utawala wa Taliban. Wahadhiri wa kiume katika vyuo vikuu walijiuzulu na baadhi ya wanafunzi wa kiume walisusia masomo yao katika kuonesha mshikamano na wanafunzi wenzao wa kike.

Tangu Taliban iliporejea madarakani Agosti mwaka 2021, Afghanistan imekuwa nchi pekee ambayo inawazuia wanawake kupata elimu.

(DPA)