1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaitaka Burundi kukomesha mzunguko wa machafuko

Saleh Mwanamilongo
15 Julai 2020

Tume ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi wa haki za binadamu Burundi inasema baada ya kipindi cha kampeni za uchaguzi,hivi sasa Burundi iko njia panda.

Wanamgambo wa Imbonerakure chama tawala nchini Burundi.
Wanamgambo wa Imbonerakure chama tawala nchini Burundi.Picha: Getty Images/AFP/C. de Souza

Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inayoichunguza Burundi imeitaka serikali mpya ya nchi hiyo kukomesha mzunguko wa machafuko unaoambatana na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na kuanza kushirikiana na tume hiyo.

Ikiwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva, Uswisi, tume ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi wa haki za binadamu nchini Burundi inasema baada ya kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu, hivi sasa Burundi iko njia panda.

Doudou Diene mwenyekiti wa jopo hilo la uchunguzi nchini Burundi anasema ingawa kwenye uchaguzi huo uliopita hakukuripotiwa machafuko makubwa, mchakato mzima wa uchaguzi ulitawaliwa na hali ya kutovumiliana kisiasa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kabla na wakati wa kampeni rasmi, siku ya uchaguzi na baada ya kutangazwa rasmi kwa matokeo.

''Mabadiliko haya ya uongozi yanaweza kuwa ni fursa ya kihistoria ya kuimarisha haki za binadamu nchini Burundi, endapo serikali itachukua hatua muafaka kuzishughulikia.Jumuiya ya kimataifa lazima isalie kuwa makini na kujipanga kuchunguza hatua ambazo zinashughulika na viongozi wapya”,alisema Diene.

Rais mpya atakiwa kuchukuwa hatua muhimu

Tume hiyo ya Umoja wa Mataifa imemuomba Rais mpya wa Burundi, Evarsite Ndayishimiye kuonyesha utashi wa kuleta mabadiliko kwa kutoa ushirikiano kikamilifu kwa mchakato wa kimataifa wa haki za binadamu. Na vilevile kuifungua tena ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu iliyofungwa mjini Bujumbura na serikali ya mtangulizi wake Pierre Nkurunziza.

Rais mteule Evariste Ndayishimishe akiapishwa mjini Gitega,Burundi.Picha: Getty Images/AFP/T. Nitanga

Wajumbe wa tume hiyo wameionya jumuiya ya kimataifa dhidi ya kulegeza msimamo mapema kana kwamba uchaguzi na mabadiliko ya kiasa yanatosha kuhakikisha moja kwa moja uimarishaji wa hali ya haki za binadamu katika kusonga mbele.

Tume hiyo inasisitiza kwamba sera za rais mpya zitatekelezwa na serikali inayoundwa na mzunguko wa mtangulizi wake, Pierre Nkurunziza ikiwemo baadhi ya watu ambao wako chini ya vikwazo kwa kujihusisha kwao na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Tume hiyo itawasilisha ripoti yake ya mwisho kwenye Baraza la Haki za Binadamu Septemba mwaka huu.

Wakati huo huo, shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, linaipongeza hatua ya Rais Ndayishimiye ya kulishughulikia janga la virusi vya corona baada ya miezi kadhaa ya kukana kuwepo kwa ugonjwa huo. Kwenye barua kwa rais Ndayishimiye, shirika la Human Rights Watch linamtaka achukuwe hatua nane muhimu katika kuimarisha haki za binadamu nchini humo mnamo kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wake. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuwafuta kazi maafisa wa jeshi waliohusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW