Umoja wa Mataifa waitaka Mali kufanya uchaguzi Februari
25 Oktoba 2021Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao uliizuru Mali kutathmini hali ya usalama, umetoa wito kwa viongozi wa serikali ya mpito kupanga tarehe ya uchaguzi utakaofanyika mwezi Februari.
Wito huo utawezesha utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS baada ya mapinduzi ya mwaka uliopita.
Ujumbe huo ulioongozwa na Balozi wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa, Martin Kimani, mwishoni mwa juma ulikutana na wadau muhimu katika makubaliano hayo.
Akizungumza na waandishi habari hapo jana mjini Bamako, Balozi Kimani amesema wameguswa na matakwa ya wananchi wa Mali kuhusu mageuzi ya kisiasa na kikatiba na kwa sasa wanasubiri kumalizika kwa kipindi cha mpito ambacho kinapaswa kuielekeza nchi hiyo katika uchaguzi.
Hata hivyo viongozi wa mpito wa Mali wamesema watathibitisha tarehe ya uchaguzi baada ya kufanyika mazungumzo ya mwezi Desemba miongoni mwa makundi yanayohusika.