1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waituhumu Syria kwa mauaji

9 Februari 2016

Tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa juu ya Syria imetoa mapendekezo ya kutaka vitangazwe vikwazo dhidi ya maafisa wa ngazi ya juu wa Syria wanaowajibika na uhalifu wa mauaji ya wafungwa

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa juu ya Syria Staffan de Mistura
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa juu ya Syria Staffan de MisturaPicha: picture-alliance/dpa/D. Balibouse

Ripoti ya tume maalum ya uchunguzi juu ya Syria pia imetaja juu ya mauaji ya watu wengi yaliyofanywa na kundi la wanamgambo wa itikadi kali la Dola la Kiislamu pamoja na kundi linalofungamana na mtandao wa Alqeda nchini Syria la Al Nusra Front.

Kimsingi jopo hilo la Umoja wa Mataifa limeweka bayana kwenye ripoti yake kwamba makundi mbali mbali yamehusika kuua maelfu ya wafungwa tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipoanza nchini Syria mwaka 2011 mnamo mwezi Marchi.Ripoti hiyo imetolewa sambamba hapo jana na ziara ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini Ankara ambako walifanya mazungumzo na waziri mkuu Ahmet Davutoglu na baadae kukutana na waandishi wa habari na kutangaza kilichoafikiwa katika mkutano wao.

Miongoni mwa masuala makubwa yaliyotajwa kufikiwa ni pamoja na ushirikiano wa nchi hizo mbili Uturuki na Ujerumani kutafuta njia za kuishinikiza jumuiya ya kujihami ya Nato kuwa mwangalizi katika mpaka kati ya Uturuki na Ugiriki kwenye eneo la bahari ya Mediterrenia.Kansela Merkel pia alibaini kwamba matumizi ya nguvu yanayoonyeshwa na Urusi na Syria katika mkoa wa Aleppo yanabidi kukomeshwa.Wakati huohuo imearifiwa kwamba jeshi la Syria limekiteka kwa mara nyingine kijiji cha pili katika mkoa wa Aleppo na kulifanya jeshi hilo na washirika wake katika mapambano kukaribia kabisa kufikia mpaka wa Uturuki.

Wakimbizi wa Syria mkoani AleppoPicha: picture alliance/AA/A. Muhammed Ali

Wakati huohuo maelfu ya wasyria wanaoyakimbia mapigano wamekusanyika katika mpaka wa Uturuki huku serikali ya Uturuki ikikhofia kwamba mapigano makali yanayoongezeka katika mkoa wa Aleppo yanaweza kuchochea watu wengi kuzidi kuyakimbia makaazi yao na kukimbilia kwenye mpaka huo wa Uturuki.

Serikali ya Uturuki inakhofia kwamba mapigano makali yanayoendelea Aleppo yanaweza kuifanya idadi ya wanaokimbilia kwenye mpaka wake ikafikia watu 60,000 ameeleza hayo naibu waziri mkuu Nurman Kurtulmus akitaja kuwa hilo litakuwa ni tukio kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa.Kundi kubwa kabisa la wakimbizi wengi wakiwa ni wanawake na watoto wamelazimika kupiga kambi katika mpaka wa Onvupinar ambao bado umefungwa lakini wakifunguliwa watu walio na mahitaji ya dharura ya huduma za afya.

Mapigano makali kaskazini mwa mkoa wa Aleppo yaliyochochewa na mashambulizi ya wiki nzima ya vikosi vya serikali vikisaidiana na ndege za kivita za urusi yameshababisha mamia kwa maelfu ya watu kuachwa bila makaazi,ambapo inatajwa kiasi watu 200,000 wamelazimika kutoroka .

Mandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman