1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Wakimbizi wa Rohingya hawawezi kurudi Myanmar

17 Agosti 2022

Kamishna mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amesema bado sio salama kwa wakimbizi wa Rohingya kurejea makwao nchini Myanmar.

Rohingya Flüchtlingslager in Bangladesch
Picha: Emre Ayvaz/AA/picture alliance

Akizungumza Jumatano na waandishi habari katika mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka, Bachelet amesema kwa bahati mbaya hali ya sasa kuzunguka mpaka inaonesha kwamba mazingira sio salama kwa watu hao kurejea, ikiwa ni karibu miaka mitano baada ya ukandamizaji uliofanywa nchini humo na kuchochea mmiminiko mkubwa wa watu kuingia nchi jirani ya Bangladesh. 

Bachelet: Watu warejeshwe kwa hiari

"Utaratibu wa watu kurejeshwa makwao unapaswa ufanywe kwa hiari na kwa njia ya heshima kwa kuzingatia utu, wakati tu patakapokuwa na mazingira salama na endelevu nchini Myanmar," alifafanua Bachelet.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa yuko Bangladesh kwa ziara ya siku nne, kabla ya kumaliza muda wake kama kamishna wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa baadae mwezi huu.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Bangladesh, Sheikh Hasina amemueleza Bachelet kwamba maelfu ya wakimbizi wa jamii ya watu wachache ya Rohingya wanapaswa kurejea Myanmar. 

Michelle Bachelet akiwa katika mkutano na Waziri Mkuu wa Bangladesh, Sheikh HasinaPicha: Samir Kumar Dey/DW

Hasina amesema wakimbizi hao wanaishi kwenye kambi za wakimbizi zilizofurika watu nchini Bangladesh. Waziri huyo mkuu wa Bangladesha amesema Warohingya ni raia wa Myanmar na wanatakiwa kurejeshwa makwao.

Bachelet aliyewasili Dhaka siku ya Jumapili, amezitembelea kambi za wakimbizi wa Rohingya katika wilaya ya Cox Bazar iliyoko karibu na mpaka wa Myanmar.

Warohingya milioni moja wanaishi Bangladesh

Takribani watu milioni moja hasa wa jamii ya Waislamu walio wachache wanaishi katika makaazi duni ya wakimbizi karibu na pwani ya kusini mwa Bangladesh.

Wengi wao waliyakimbia maakazi yao baada ya ukandamizaji wa jeshi la Myanmar mwaka 2017, ambalo sasa linakabiliwa na kesi ya kihistoria kuhusu mauaji ya kimbari katika mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa.

Miaka mitano baadae, wakimbizi wanakataa kurejea nyumbani kutokana na kutohakikishiwa kuhusu usalama wao pamoja na haki zao Myanmar, nchi ambayo kwa sasa inatawaliwa na jeshi baada ya kuondolewa madarakani serikali ya kiraia mwaka uliopita.


(AFP, AP)
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW