1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa walaani bomoa bomoa ya Kibera

27 Julai 2018

Operesheni ya kuwahamisha watu kutoka makazi ya Kibera, jijini Nairobi imezusha kelele na lawama kutoka pande mbalimbali. Watalaamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameitaka Kenya isitishe zoezi hilo mara moja.

Kenia Häuser im Kibera slum in Nairobi müssen einer neuen Straße weichen
Picha: Reuters/B. Ratner

Kulingana na taarifa liyochapishwa kutoka kwenye ofisi ya kamishna wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki za binadamu OHCHR kwa vyombo vya habari, zoezi hilo lililoanza alfajiri ya tarehe 23 mwezi huu wa Julai litawaathiri zaidi ya wakazi elfu 30 ambao wataachwa bila makao. Hadi kufikia sasa tangu operesheni hiyo ilipoanza takriban watoto 2000 hawaendi shule.

Wataalamu wa kutetea haki za binadamu wa shirika la Umoja wa Mataifa OHCHR wamelaani vitendo vya kuwatoa maelfu ya watu majumbani mwao kwenye eneo hilo la mabanda la Kibera lililo kusini magharibi mwa jiji la Nairobi. Watalaamu hao wa Umoja wa Mataifa wanaitaka serikali ya Kenya isitishe zoezi hilo mpaka pale utaratibu wa kisheria na usalama wa kutosha utakapofanyika.

Rais wa Kenya Uhuru KenyattaPicha: imago/i Images

Bomoa bomoa hiyo imefanyika kinyume na makubaliano ya hapo awali kati ya Mamlaka ya barabara za mijini Kenya Urban Roads Authority, KURA, Tume ya kitaifa ya ardhi na Tume ya kitaifa ya haki za binadamu nchini Kenya, KNCHR. Operesheni hiyo ilianzishwa bila ya kutolewa taarifa ya mapema na bila ya kuwepo na mpango wowote wa kuwapatia watu makazi mbadala.

Wataalamu wa kutetea haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wanasisitiza kwamba serikali ya Kenya ifuate sheria kuhusu njia sahihi za kuwahamisha watu kwa mashauriano na ushirikiano kwa ajili ya maendeleo kulingana na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu kama inavyopendekezwa na kamati za kiuchumi, kijamii na kitamaduni.

Mwandishi: Zainab Aziz/Press Release

Mhariri: Mohammed Khelef