Umoja wa Mataifa walaani kubomolewa turathi za Iraq
6 Machi 2015Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Paris hivi leo, mkuu wa shirika linaloshughulikia utamaduni kwenye Umoja wa Mataifa alisema kitendo kilichofanywa na Dola la Kiislamu kwenye makumbusho moja huko Iraq ni sawa na "maangamizi dhidi ya utamaduni"
"Ni maangamizi dhidi ya utamaduni. Hakuna neno jengine la kuelezea kile kinachotokezea. Ni maangamizi ya wazi dhidi ya utamaduni. Kwa kusema ukweli, sikuweza kuziangalia picha za maangamizi hayo hadi hapo jana. Zilikuwa zinatisha. Zinaogofya hasa. Sikuweza kuziangalia mpaka mwisho." Alisema Irina Bokova, mkurugenzi mkuu wa UNESCO, akisisitza kuwa vitendo hivyo ni sawa na uhalifu wa kivita na akitoa wito kwa dunia iwaadhibu wale walioutenda.
Msimamo huu wa UNESCO ulikuja siku moja tu baada ya vidio kusambazwa mitandaoni ikiwaonesha wanamgambo wa Dola la Kiislamu wakiharibu vitu vya kale vya zama za Mesopotomia katika makumbusho moja mjini Mosul, mji wa pili kwa ukubwa nchini Iraq.
Jengo la kale Nimrud laangushwa
Taarifa kutoka mji wa kale wa zama za Assyria wa Nimrud zinasema wanamgambo hao waliliangusha jengo jengine lenye umri wa miaka 3,000 kwenye Mto Tigris. Mji wa Nimrud ulio umbali wa kimolita 30 kusini mwa Mosul, ulijengwa miaka 1250 kabla ya kuzaliwa Kristo.
Ni mji huo ambao karne nne baadaye ulikuja ukawa makao makuu ya dola ya Assyria, ambalo kwa wakati huo ndilo lililokuwa dola lenye nguvu kabisa duniani, likitawala kutokea Misri ya leo, hadi Uturuki na Iran.
Ubomoaji huo ulikuwa ni sehemu ya kampeni ya kundi hilo la siasa kali ambalo hadi sasa limeshaharibu maeneo kadhaa matukufu na ya kihistoria, zikiwemo nyumba za ibada za Waislamu, katika kile wanachosema ni kuteketeza uzushi kwenye Uislamu.
Iraq yaomba silaha zaidi kunusuru turathi zake
Balozi wa Iraq kwenye shirika hilo la UNESCO, Mahmoud Khalaf, amelitolea wito Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuipa nchi yake msaada wa kijeshi ili kuwazuia wanamgambo wa Dola la Kiislamu wasiendelee na uharibifu wao wa turathi za kilimwengu zilizoko Iraq.
"Tunadhani kukanusha na kulaani tu hakutoshi. Tunalitaka Baraza la Usalama na nchi zote duniani kushirikiana na Iraq, kutusaidia kwa silaha. Madhali Mosul au sehemu nyengine yoyote ya Iraq imekaliwa na kundi hili la uharibifu, uhalifu utaendelea na alama na turathi za Iraq zitateketezwa zote," alisema Khalaf akiwa mjini Paris kushiriki kikao na wakuu wa UNESCO.
Kiongozi wa al-Nusra Front auawa
Hayo yakiendelea, kundi la al-Nusra Front ambalo ni tawi la al-Qaida nchini Syria limempoteza kamanda wake mkuu, Abu Hammam al-Shami, sambamba na viongozi wengine kadhaa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali na waangalizi wa haki za binaadamu walioko huko, Abu Hammam aliuawa kwenye operesheni maalumu ya kijeshi katika jimbo la Idlib, ingawa hakuna tarehe iliyotajwa kufanyika operesheni hiyo.
Mkurugenzi wa Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu la Syria, Rami Abdel Rahman, alithibitisha kuuawa kwa kamanda huyo ingawa naye hakuelezea mazingira ya kifo chake.
Rami ameliambia shirika la habari la AFP kwamba huenda Shami ni miongoni mwa viongozi waliojeruhiwa kwenye mashambulizi ya anga yaliyofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani huko Idlib mnamo tarehe 27 Februari.
Hiyo ni siku ambapo mtandao rasmi wa al-Nusra ulitangaza kuuawa kwa viongozi wake wawili, lakini haukuwa umechapisha majina ya waliouawa.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Josephat Charo