1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa walaani mauaji dhidi ya wasichana Libya

Daniel Gakuba
20 Machi 2020

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya umelaani mashambulizi yaliyowauwa wasichana watano. Mauaji hayo yametokea wakati miito ya kimataifa ikitolewa kuzitaka pande zinazohasimiana Libya kusitisha uhasama.

Libyen Freischärler mit Waffen
Picha: picture-alliance/dpa

Katika tangazo lake lililotolewa kupitia mtandao wa twitter, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umesema waliouawa katika mashambulizi hayo ni wasichana watano wenye umri wa kati ya miaka 14 na 20, na kuongeza kuwa wengine pia watano, akiwemo mwenye umri wa miaka 11, wamejeruhiwa.

Tangazo hilo limesema vifo hivyo na majeraha vimetokana na mashambulizi ya mizinga iliyofyatuliwa kiholela katika kitongoji cha makaazi ya watu cha Ain Zara, ambayo yanashukiwa kufanywa na vikosi vitiifu kwa mbabe wa kivita Khalifa Haftar, vijulikanavyo kama Jeshi la Taifa la Libya, LNA.

Vikosi hivyo vyenye makao yake mashariki mwa Libya vimekuwa vikiendesha operesheni ya karibu mwaka mzima, kwa lengo la kuukamata mjini mkuu wa nchi hiyo, Tripoli kutoka mikononi mwa serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Ingawa Libya haijathibitisha kisa chochote cha maambukizi ya virusi vya corona, Shirika a Afya Ulimwenguni WHO limetoa tahadhali, na kuonya kuwa nchi hiyo inayokumbwa na mizozo ya muda mrefu, haiku tayari kukabiliana na mripuko wa virusi hivyo.

Jumanne wiki hii, nchi kadhaa za Magharibi na za Kiarabu, zikiwemo zile zinazounga mkono pande tofauti katika mzozo wa Liba, zilizitolea mwito pande zote katika mzozo huo kusimamisha mapigano, na kuelekeza juhudi katika kujilinda dhidi ya virusi vya corona.

Miito kama hiyo ilitolewa pia na Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Ulaya.

Hadi sasa hakuna mafaniko makubwa ya kidiplomasia yaliyopatikana, katika juhudi za kutafuta suluhisho la kisiasa kwa ghasia zinazoisibu Libya, ambazo zimeendelea kuwepo tangu kuangushwa kwa utawala wa Muamar Gaddafi mwaka 2011.

Mapema mwezi huu, mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya Ghassan Salame alijiuzulu wadhifa huo, akisema mfadhaiko wa mawazo uliotokana na kazi hiyo ulikuwa ukiathiri vibaya afya yake. Salame aliachia ngazi wakati mazungumzo baina ya mahasimu wa nchini Libya yanafanyika mjini Geneva yakisuasua, sambamba na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotiwa Saini mwezi Januari.

Awali alikuwa amelalamikia kukiukwa kwa vikwazo vya silaha kwa Libya, ambapo pande zote katika mzozo wa nchi hiyo zilikuwa zikiendelea kupokea shehena za silaha.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya Ghassan Salame Picha: Reuters/D. Balibouse

Upande wa Jenerali Khalifa Haftar unaungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Urusi, huku serikali ya mjini Tripoli inayoongozwa na waziri Mkuu Serraj al-Faiz, ikisaidiwa na Uturuki.



Vyanzo rtre, ape