Umoja wa Mataifa walaani Taliban "kuwakandamiza" wanawake
28 Aprili 2023Azimio hilo limepitishwa kwa sauti moja na wanachama wote 15 wa Baraza la Usalama na limewatolea mwito viongozi wa Taliban kubadili mkondo wa kile azimio hilo limekitaja kuwa "ukandamizaji wa haki za wanawake na wasichana."
Mapema mwezi huu, utawala wa Taliban ulianza kutekeleza amri ya kuwazuia wanawake nchini Afghanistan kufanya kazi na taasisi za Umoja wa Mataifa, uamuzi uliozusha ukosoaji mkubwa kutoka Jumuiya ya Kimataifa.
Azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitaja hatua hiyo kuwa ni ukandamizaji wa haki za binadamu na misingi ya utu.
Azimio hilo limesema kitendo cha kuwazuia wanawake kufanya kazi na taasisi za Umoja wa Mataifa kinarudisha nyuma nafasi ya wanawake katika jamii ya Afghanistan.
Wanadiplomasia wasema ulimwengu hautafumbia macho ukandamizaji Afghanistan
Kupitia azimio hilo, Baraza la Usalama limetoa wito kwa mataifa na taasisi zote duniani kutumia ushawishi walionao kushinikiza kubadilishwa kwa sera na matendo ya utawala wa Taliban yanayotia kiwingu upatikanaji wa haki za binadamu.
Wakizungumza baada ya kupitishwa azimio hilo mabalozi wa mataifa yaliyoshiriki wamesema ulimwengu hautafumbia macho madhila wanayopitia wanawake nchini Afghanistan chini ya utawala wa Taliban.
Balozi wa kudumu wa Umoja wa Falme za Kiarabu katika Umoja wa Mataifa Lana Zaki amesema "Dunia haitakaa kimya wakati wanawake wa Afghanistan wanafutwa katika jamii".
Kwa upande wake Naibu Balozi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Robert A. Wood amesema, "Marekani ingependa kutambua ujasiri wa wanawake na wasichana wa Afghanistan. Licha ya vizuizi na vitimbi vya Taliban, wameendelea kuzisaidia familia zao na kutoa mchango kwenye jamii yao. Tunazisifu pia jamii za Waafghani na raia mmoja mmoja waliosimama kwa ushujaa kuwaunga mkono wanawake na wasichana wa Afghanistan"
Urusi yaikalia kooni Marekani kuhusu fedha za Afghanistan
Urusi kupitia mwanadiplomasia wake ilipiga kura ya Ndiyo kuunga mkono azimio hilo, lakini ilikwenda mbali zaidi kwa kuyalaumu mataifa ya magharibi kuikwamisha Afghanistan.
Balozi wa Urusi, Vasily Nebenzia alisema iwapo Marekani inataka kuonesha nia thabiti ya kuisaidia Afghanistan, inapaswa kuacha kuzishikilia mali Afghanistan ikiwemo kitita cha dola bilioni 7 za Benki Kuu ya Afghanistan zilizozuiwa na Washington baada ya Taliban kuchukua madaraka mwaka 2021.
Kura ya kupitisha azimio hilo la kuukosoa utawala wa Taliban imepigwa ikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufanyika mkutano wa kimataifa kuhusu Afghanistan.
Mkutano huo ulioitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres utafanyika mjini Doha mnamo tarehe 1 na 2 mwezi Mei.
Utawakutanisha wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali duniani kutafuta mkakati wa pamoja wa kufikia malengo ya kuisaidia Afghanistan katika wakati taifa hilo liko chini ya udhibiti wa Taliban.