1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres atoa mwito rais Myint na Suu Kyi waachiwe huru

2 Julai 2021

Serikali ya kijeshi iliwaachia huru zaidi ya wafungwa 2000 waliokamatwa kufuatia harakati za kupinga mapinduzi ya kijeshi

Myanmar Yangon | Proteste gegen Militärregime an Geburtstag von Aung San Suu Kyi
Picha: AFP

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres siku ya Alhamisi alitowa mwito kwa jeshi la Myanmar lililotwaa kwa nguvu madaraka, kuwaachia huru mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka 1991, Aung San Suu Kyi na Rais Win Myint.

Wito wa katibu mkuu Guterres umekuja siku moja baada ya maelfu ya wafungwa wengine kuachiwa huru nchini Myammar. Eri Kaneko ambaye pia ni msemaji wa Gutteres ametoa ujumbe wa katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akisema wanachokisisitiza ni kuachiwa huru mara moja wale wote waliofungwa kiuonevu bila kufuatwa sheria ikiwa ni pamoja na rais Win Myint na kiongozi mkuu wa nchi Aung San Suu Kyi.

Picha: AFP

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, mnamo siku ya Jumatano watu zaidi ya 2000 waliokuwa wamefungwa waliachiliwa huru miongoni mwao,waandishi habari na watu wengine ambao jeshi linaloshikilia madaraka limesema walifungwa kutokana na mashtaka ya kuhusika na uchochezi kufuatia kitendo cha kushiriki kwenye maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi.

Myanmar iko kwenye mkwamo mkubwa tangu jeshi lilipotwaa madaraka kwa nguvu Feb 1 kuiondoa serikali iliyochaguliwa kwa njia ya demokrasia ya Aung San Suu Kyi.

Wengi wa watu wanaolipinga jeshi wanashikiliwa, baadhi wameshtakiwa chini ya sheria inayosema ni uhalifu kutoa tamko lolote linaloweza kusababisha hofu au kueneza habari za uwongo.

Kiongozi wa kiraia Suu Kyi anashtakiwa kwa tuhuma za kufanya kosa kama hilo miongoni mwa mengine na bado anashikiliwa jela. Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kaneko amesema wana wasiwasi mkubwa na muendelezo wa machafuko na vitisho ikiwa ni pamoja na hatua ya watu kukamatwa ovyo bila ya ushahidi na vikosi vya usalama.

Picha: REUTERS

Lakini pia hapo jana mahakama ya Myanmar ilirefusha kipindi cha kumuweka kizuizini mwandishi habari wa jarida la Fontier Myanmar, Danny Fenster wakati akisubiri kesi yake isikilizwe.

Fenster ni mhariri msimamizi raia wa kimarekani aliyeajiriwa na jarida hilo la habari la mtandaoni katika nchi hiyo ya Kusini Mashariki mwa Asia. Alikamatwa mwezi Mei katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Yangon kwa tuhuma za uchochezi, kosa ambalo hukumu yake ni hadi miaka mitatu gerezani.

Mwandishi habari huyo jana Alhamisi akifikishwa mahakamani alionesha kupungua mwili lakini binafsi akasema kwamba yuko salama. Kesi hiyo ya tuhuma za uchochezi dhidi ya Daniel iliakhirishwa hadi Julai 15 kwa mujibu wa wakili wake.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW