1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waombwa kusimamia mazungumzo ya amani Syria

3 Novemba 2017

Kundi moja kubwa la upinzani nchini Syria kupitia kamati yake kuu ya Majadiliano, HNC limetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kusimamia tena mchakato wa mazungumzo ya kutafuta amani nchini Syria.

Schweiz Friedensverhandlungen für Syrien
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Di Nolfi

Kundi moja kubwa la upinzani nchini Syria limetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kusimamia tena mchakato wa mazungumzo ya kutafuta amani nchini Syria. Hii ni baada ya Urusi kutangaza kuwa itaandaa mazungumzo tofauti baadaye mwezi huu, wakati huu hatima ya mazungumzo yanayoisha leo mjini Astana, Kazakhstan, ikiwa haifahamiki.

Kamati Kuu ya Majadiliano, HNC, kama liliijitavyo kundi hilo, linasema Urusi inauhujumu Umoja wa Mataifa kwa kulazimisha sheria zake kwa Syria ambako watu 400,000 wameuawa katika vita vya miaka sita vya wenyewe kwa wenyewe.

Urusi ni mshirika wa dhati wa rais wa Syria, Bashar Assad, na imetuma usaidizi wa majeshi ya angani pamoja na washauri wa kijeshi kulisaidia jeshi la Syria kupambana na waasi wenye silaha pamoja na wapinzani wengine, huku Urusi ikisema inapiga vita ugaidi.

HNC yasema haitashiriki mazungumzo bila Umoja wa Mataifa

Kupitia taarifa yake, HNC imesema haitashiriki katika shughuli yoyote itakayoandaliwa nje ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, huku ikiilaumu Urusi kwa kuibeba serikali ya Syria.

Mwanajeshi wa Urusi katika helikopta inayopaa katika anga ya Palmyra,SyriaPicha: picture alliance/AP Photo

Kauli ya HNC inakuja huku majaaliwa ya mazungumzo ya siku tatu yaliyoanza juzi mjini Astana, nchini Kazakhstan, yakiwa hayafahamiki. Mazungumzo hayo ambayo yaliitishwa kwa ushirikiano wa Uturuki, Urusi na Iran, yalitazamiwa kuwakusanya pamoja makundi na vyama vya siasa 33 vya Syria, pamoja na serikali na washirika wa vita hivyo vya miaka sita.

Muungano huo wa kitaifa wa Syria ambao ni kundi la upinzani lenye makao yake Uturuki na ambalo ni tawi la kisiasa la waasi wenye silaha, kwa jina jingine Free Syrian Army, umesema hautashiriki katika mazungumzo ambayo yamependekezwa kufanyika Sochi. Akizungumzia mzozo wa syria rais wa Urusi, Vladmir Putin, alisema: "Bado yapo maswali na matatizo kuhusu Syria na hakuna linaloweza kusuluhishwa na nchi moja. Hakuna upande au nchi inayoweza kutatua mzozo wa Syria kivyake."


Mazungumzo ya Sochi

Umoja wa Mataifa haujasema ikiwa utashiriki mazungumzo hayo ya Sochi ya Novemba 18, siku kumi kabla ya Umoja huo kuandaa mkutano kati ya serikali na upinzani mjini Geneva.

Rais wa syria Bashar AssadPicha: picture-alliance/AP Photo/Syrian Presidency

Mazungumzo ya Sochi yatafungua duru ya nne ya mazungumzo kati ya pande husika ambazo zimehusika mno katika machafuko ya Syria. Mpangilio wa Umoja wa Mataifa pia umechangiwa pakubwa na mazungumzo ya kimkakati ya Astana ambayo yamekuwa yakisimamiwa na Iran, Uturuki na Urusi, ambao wote ni washirika wa kimataifa katika vita vya Syria.

Urusi ilifungua duru ya tatu ya mazungumzo kupitia Cairo. Misri imewapa kambi waasi waliobadili nia na kuonekana kuikubali serikali ya Damascus. Lakini kwa msingi kuwa udhibiti wa madaraka unapendelea Assad kufuatia usaidizi mkubwa wa kijeshi kutoka Urusi, mazungumzo hayajazalisha matokeo imara, na hivyo kupelekea waasi kuilaumu Urusi na Damascus kwa kukwamisha hali

HNC inayoungwa mkono na mataifa ya Magharibi pamoja na makundi mengine ya waasi, imetaka kuwa mchakato wowote uwe katika mfumo wa kisheria chini ya Azimio Namba 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalozungumzia kipindi cha mpito cha kisiasa.

Makundi mengine yanayoongozwa na Hay'at Tahrar na al-Sham ambayo yana ufungamano na mtandao wa al-Qaeda yamekataa mazungumzo ya amani na serikali ya Assad.

Mwandishi: John Juma/APE

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW