1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waongeza muda wa ujumbe wake Libya

30 Aprili 2022

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kwa kauli moja kuongeza muda wa ujumbe wa kisiasa wa umoja huo nchini Libya kwa muda wa miezi mitatu.

Libyen Wahl in Libyen immer unwahrscheinlicher - UN besorgt über Lage
Picha: Hamza Turkia/Xinhua/dpa/picture alliance

Kura hiyo imefanyika Ijumaa wakati ambapo Marekani na Uingereza zimeishutumu Urusi kwa kuzuia kuongezwa kwa mamlaka ya muda mrefu na madhubuti zaidi, ambayo yangejumuisha kuendeleza maridhiano ya serikali zinazohasimiana ambazo kwa sasa zote zinadai kuwa na mamlaka.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia amesema nchi yake inasisitiza kuongezwa muda wa miezi mitatu ili kumshinikiza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kumteua haraka mwakilishi mpya atakayeuongoza ujumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya unaojulikana kama UNSMIL. Mjumbe maalum wa zamani wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Jan Kubis, alijiuzulu Novemba 23, 2021 miezi 10 baada ya kushikilia wadhifa huo.

Nebenzia amesema kutokuwepo kwa mjumbe mpya, kikosi cha UNSMIL kimeshindwa kutoa msaada mkubwa unaohitajika katika mchakato wa kisiasa nchini Libya kwa zaidi ya miezi sita.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia Picha: picture alliance / NurPhoto

Mwanadiplomasia huyo wa Urusi amewalaumu baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao hajawataja na aliodai kwamba hawako tayari kukubaliana na hali halisi kwamba UNSMIL inaongozwa na mwakilishi wa Afrika, akisema upinzani wao haujengi na kwamba inadhihirisha ukoloni mamboleo.

Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, Barbara Woodward, ambaye alisimamia mazungumzo kuhusu azimio hilo, alisema baada ya kura hiyo kwamba Urusi imejitenga kwa mara nyingine tena kutokana na kutojiunga na makubaliano ya wanachama wengine 14 wa baraza hilo, ambao waliunga mkono mamlaka ya UNSMIL kuongezwa kwa muda wa mwaka mmoja.

Marekani: Mamlaka ya muda mfupi yanatatiza uwezo wa Umoja wa Mataifa

Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Jeffrey DeLaurentis amesema mamlaka ya muda mfupi yanatatiza uwezo wa Umoja wa Mataifa kumteua mkuu npya wa ujumbe wa UNSMIL na yanazusha hali ya sintofahamu kwa watu wa Libya na viongozi wao kuhusu jukumu la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nchini Libya.

DeLaurentis pia aliikosoa Urusi kwa kuondoa lugha muhimu katika mageuzi ya sekta ya maridhiano na usalama, ambayo wanachama watatu wa Kiafrika wa baraza hilo walishinikiza ijumuishwe katika azimio lililopitishwa Ijumaa.

Baada ya Kubis kujiuzulu, Guterres alimteua Stephanie Williams mwanadiplomasia raia wa Marekani, kuwa mshauri wake maalum na kumpeleka Tripoli. Williams ambaye pia anazungumza kwa ufasaha lugha ya Kiarabu, aliwahi kuwa naibu mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya kuanzia mwaka 2018 hadi 2020.

Stephanie Williams, anayekaimu nafasi ya mjumbe maalulm wa Umoja wa Mataifa nchini LibyaPicha: Martial Trezzini/KEYSTONE/picture alliance

Mwanadiplomasia huyo wa Marekani alisimamia makubaliano ya kusitisha mapigano na serikali ya mpito na aliwaambia waandishi habari baada ya mkutano wa hivi karibuni wa mahasimu wa Libya uliofanyika mjini Cairo, Misri kwamba viongozi wanaohasimiana wlaikubali kurejea tena kwenye meza ya mazungumzo mwezi Mei.

Balozi wa Gabon kwenye Umoja wa Mataifa, Michel Biang alisoma taarifa kwa niaba ya nchi yake, Ghana na Kenya akisema mgawanyiko unaoongezeka nchini Libya, katika wakati muhimu ambao unahitaji hatua za Baraza la Usalama lililoungana ili kusaidia mchakato wa amani kuwa endelevu, hali ambayo watu wa Libya wanaitamani.

Afrika yataka wanajeshi wa kigeni waondoke Libya

Nchi hizo tatu za Afrika ambazo ni wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimezitolea wito pande zinazohasimiana nchini Libya, kuweka kando tofauti zao za kisiasa na waelewa kwamba njia za kijeshi hazitaleta suluhisho endelevu la amani kwa sababu za msingi za mgogoro huo.

Gabon, Kenya na Ghana zimelaani uingiliaji wa kijeshi nchini Libya, na zimetaka kuondoka kwa wapiganaji wote wa kijeshi na mamluki na zimeutaka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na washirika wa kimataifa kuunga mkono mazungumzo ya kitaifa na maridhiano nchini Libya.

Libya, taifa la Afrika Kaskazini lenye utajiri mkubwa wa mafuta lilitumbukia katika hali ya machafuko tangu vuguvugu la mapinduzi lililoungwa mkono na Jumuia ya Kujihami ya NATO na kumuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Waziri Mkuu wa mpito wa Libya, Abdul Hamid Mohammed Dbeibah na Waziri Mkuu mpya, Fathi Bashagha

Mwaka 2014, Libya iligawanyika baina ya serikali mbili zinazopigana za mashariki inayoongozwa na kamanda wa kijeshi Khalifa Hafter na ya magharibi inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa iliyoko kwenye mji mkuu, Tripoli.

Oktoba mwaka 2020, mahasimu hao walifikia makubaliano ya amani ya kuwepo kwa serikali ya mpito ifikapo Februari mwaka 2021, na uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 24 mwaka jana haukufanyika.

Mwezi Februari, Baraza la Wawakilishi lilimteua Fathi Bashagha kuwa waziri mkuu mpya baada ya kudai kuwa mamlaka ya aliyekuwa waziri mkuu Abdul Hamid Dbeibah yamefikia mwisho.

(AP)