Umoja wa Mataifa waonya juu ya kitisho cha njaa Myanmar
22 Aprili 2021Kwa mujibu wa uchambuzi uliotolewa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) siku ya Alkhamis (Aprili 22), watu wapatao milioni 3.4 watashindwa kupata chakula cha kutosha ndani ya kipindi cha miezi mitatu hadi sita ijayo, ambapo maeneo ya mijini ndiyo yatakayoathirika zaidi, kutokana na kupoteza ajira katika sekta za ujenzi, usindikaji na huduma, huku bei za vyakula zikipanda.
Mkurugenzi wa WFP nchini Myanmar, Stephen Anderson, alisema watu wengi sana wamepoteza kazi zao na hawawezi kujinunulia hata chakula kwa siku, akitoa wito wa juhudi za haraka kuchukuliwa kuzuwia hali hiyo kuwa janga ndani ya kifupi kijacho.
Shirika hilo lilisema bei ya mchele na mafuta ya kupikia ilikuwa imepanda kwa takribani asilimia 18 mwishoni mwa mwezi Februari, huku dalili zikionesha familia kadhaa katika mji mkuu wa kibiashara, Yangon, zimeanza kuchupisha milo, zinakula vyakula vyenye lishe haba na zinazama kwenye madeni.
WFP inapanga kutanuwa operesheni zake nchini Myanmar kwa kuongeza watu milioni 3.3 katika orodha ya inaowasaidia, na kwa hali hiyo imeomba dola milioni 106 kukabiliana na kitisho hicho cha njaa.
Vikwazo vipya vya Marekani
Hayo yanakuja katika wakati ambapo wizara ya fedha ya Marekani ilitangaza vikwazo vipya vya kiuchumi dhidi ya Myanmar kwa kuziweka kampuni za biashara ya mbao na lulu kwenye orodha ya vikwazo hivyo kuanzia Jumatano (Aprili 21).
Kampuni za Myanmar Timber Enterprise na Myanmar Pearl Enterprise, zinahohusika na usafirishaji wa mbao na lulu na ambazo zina mafungamano na utawala wa kijeshi ndizo zilizowekwa kwenye orodha hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo wa Kigeni wa Marekani, Anthony Blinken, uamuzi huo ulikuwa unatuma ujumbe wa wazi kwa utawala wa kijeshi nchini Myanmar kwamba utaendelea kuandamwa na mbinyo wa kimataifa kutokana na kitendo chake cha kuzima matakwa ya wananchi na kutumia nguvu dhidi ya raia wasiokuwa na silaha.
Vikwazo hivyo vinazizuwia kampuni hizo kutokufanya biashara zake kwenye mifumo ya kilimwengu ya kibiashara na kifedha na pia kuwazuwia raia na kampuni za Marekani, zikiwemo benki zenye mafungamano na Marekani, kufanya nayo kazi.
Vikwazo hivyo pia vinazizuwia mali zote zinazomilikiwa na kampuni hizo nchini Marekani.
"Marekani itaendelea kuwaunga mkono raia wa Myanmar katika jitihada zao za kuyakataa mapinduzi ya kijeshi, na wakati huo huo kuutolea wito utawala wa kijeshi kuacha matumizi ya nguvu, kuwaachia wafungwa wote na kuirejesha nchi katika njia ya demokrasia." Alisema Blinken.