1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu baa la njaa Yemen

24 Oktoba 2018

Mkuu wa masuala ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock ameonya kuwa Yemen iko katika hatari kubwa ya kukumbwa na baa la njaa.

Jemen |  Unterernährtes Kind
Picha: picture-alliance/dpa/AA/M. Hamoud

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Lowcock amesema kuwa nusu ya wananchi wa Yemen wako katika hatari ya kukabiliwa na uhaba wa chakula na huenda wakategemea misaada kwa ajili ya kuishi. Amesema watu milioni 14 wanahitaji msaada wa chakula na siyo watu milioni 11 kama ilivyokadiriwa mwezi uliopita.

''Hiyo ni nusu ya idadi jumla ya watu wa nchi hiyo. Na pili, wakati mamilioni ya watu wanategemea msaada wa chakula cha dharura kwa miaka mingi, msaada wanaoupata unawasaidia tu kuishi na sio kwa ajili ya kuwapatia afya,'' alisema Lowcock.

Amebainisha kuwa hali hiyo inatisha kuliko onyo la uhaba wa chakula nchini Yemen, lililotolewa mwanzoni mwa mwaka uliopita wa 2017 na pia mwezi Novemba na kwamba mzozo wa kibinaadamu nchini Yemen ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia.

Watoto wa Yemen wakisubiri kupatiwa msaada wa chakulaPicha: picture-alliance/Photoshot/M. Mohammed

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema njia pekee ya kulizuia janga hilo la njaa ni kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano kwenye maeneo yanayohitaji msaada wa kibinaadamu pamoja na kuruhusu meli zenye msaada kuingia nchini humo kupitia bandari ya Hodeidah. Lowcock amesema bandari hiyo ni muhimu kwa sababu Yemen inaingiza nchini humo kiasi ya asilimia 90 ya chakula.

Aidha, amezishutumu pande zinazohasimiana kwa kukiuka sheria ya kimataifa kuhusu ubinaadamu, hali inayozuia misaada kupelekwa. Lowcock ameuambia mkutano huo uliopendekezwa na Uingereza kutokana na kuendelea kuzorota kwa hali ya kiusalama nchini Yemen, kwamba tangu Umoja wa Mataifa ulipotoa tahadhari mwezi Septemba, hali nchini Yemen imezidi kuwa mbaya.

Tangu mwaka 2015, mzozo wa Yemen umesababisha vifo vya kiasi ya watu 10,000. Umoja wa Mataifa umewahi kutangaza mara mbili tu kuhusu janga la uhaba wa chakula ndani ya kipindi cha miaka 20, moja likiwa ni lile la Somalia mwaka 2011 na jengine mwaka uliopita katika baadhi ya maeneo ya Sudan Kusini, hatua inayoifanya hali ya Yemen kuwa ya kutisha.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, DPA, AFP, Reuters
Mhariri: Iddi ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW