Umoja wa Mataifa waonya kuhusu Somalia
14 Septemba 2010Pia Umoja huo ukiitaka serikali dhaifu ya mpito nchini Somalia kuachana na migogoro. Suala la Somalia litakuwa katika agenda katika mkutano wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi, na wik,i ijayo itakuwa zamu ya Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuijadili hali nchini Somalia katika mkutano wa mawaziri.
Katika ripoti kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja huo Ban Ki-moon alitoa mfano wa shambulizi la kujitoa mhanga lililofanyika Uganda mwezi Julai- kama ishara kuwa kundi la Al-Shabab linapanua mbawa zake za vitisho katika maeneo mbali mbali.
bWatu 70 waliuawa katika miripuko hiyo miwili ya bomu, na Ban Ki-moon alisema hii iliashiria wazi kuwa tishio la wanamgambo hao wenye itikadi kali haliko tu Somalia, bali katika nchi jirani na vile vile katika jumuiya ya kimataifa. Miongo miwili ya vita, umwagaji damu na mgogoro imelitumbukiza taifa hilo la Somalia katika mgogoro mkubwa, lakini kuibuka kwa kudni la Al-Shabab imeongeza maji unga na inawatia wasiwasi nchi za magharibi. Na usisahau pia lile bughdha la uharamia.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa iliendelea kusema, wanajeshi 7,200 wa Umoja wa Afrika wanaojulikana kama AMISOM ndio wanaowazuia Al-Shabab wasiuteke kabisa mji mkuu Mogadishu. Katika mwaka huu tu maelfu ya watu wameuawa mjini Mogadishu, huku Umoja wa Mataifa ukionya kuwa huduma za afya katika mji huo zinakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwahudumia waathiriwawanaojikuuta taabani baada ya mashambulizi.
Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Augustine Mahiga, pamoja na mjumbe wa Umoja wa Afrika Boubakar Diarra na mjumbe mwingine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kipruto Arap Kirwa walinusurika kifo wiki iliopita, baada mshambulizi wa kujitoa mhanga kujilipua katika uwanja wa ndege muda mfupi tu baada ya wajumbe hao kumaliza mkutano na Rais Sheikh Sharrif. Watu watano waliuawa katika shambulizi hilo.
Wajumbe hao walionya kuwa serikali hiyo ya mpito inakabiliwa na mizozano ya ndani kwa ndani, na kwamba hili linaatjiri juhudi za kumaliza mzozo huo wa Somalia.
Serikali hiyo ya mpito inamaliza muda wake Agosti 2011, lakini kulingana na wataalam hadi sasa hawajafanikiwa kufanya lolote nchini humo, huku mivutano ya kisiasa ikisababisha Rais Sharrif kulivunjilia mbali baraza la mawaziri, na spika wa bunge kujiuzulu.
Katika ripoti yao, baada ya ziara yao, wajumbe hao watatu walisema wanajeshi wa Somalia na vikosi vya AMISOM wanahatarisha maisha yao kila siku wakijaribu kuilinda serikali hiyo ya mpito na juhudi hizo za amani, Somalia.
Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE
Mhariri: Abdul-Rahman