1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu 'uhalifu wa kivita' Tigray

13 Novemba 2020

Umoja wa Mataifa umeonya kwamba kuna uwezekano kuwa uhalifu wa kivita umefanywa nchini Ethiopia katika jimbo laTigray.

Schweiz Genf | UN-Hochkommissarin |  Michelle Bachelet
Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Umoja wa Mataifa UNCHR Michelle Bachelet ametaka uchunguzi kamili ufanywe kufuatia ripoti ya mauaji ya halaiki katika mji wa Mai-Kadra, ambapo shirika la Amnesty International lilisema limethibitisha kidijitali picha na video zilizoonyesha miili iliyotapakaa katika mji huo ikiondolewa kutumia machela.

Kwenye taarifa, Bachelet amesema ikiwa itathibitishwa kwamba mauaji hayo yamefanywa makusudi na upande wowote kufuatia machafuko ya sasa hivi, basi mauaji hayo ya raia yatakuwa yamefikia kiwango cha kuitwa uhalifu wa kivita.

Mamia ya watu wameripotiwa kuuawa, wengine kwa njia za kikatili. Kulingana na shirika la Amnesty International iliyoongeza kwamba maelfu ya watu katika jimbo hilo wamekimbia Tigray, jimbo ambalo Abiy anawatuhumu viongozi wake kwa kutaka kuiyumbisha nchi.

Abiy apongeza jeshi kukomboa magharibi mwa Tigray

Waziri Mkuu Abiy Ahmed amevipongeza vikosi vyake kwa kukomboa baadhi ya maeneo katika jimbo hilo.

"Mashujaa wanajeshi wa Ethiopia wamezuia na kuharibu mpango wa kundi la TPLF kuchukua udhibiti wa baadhi ya kambi za kijeshi na hifadhi za silaha katika kamandi ya Kaskazini. Pia tumeweza kudhibiti silaha na zana za nzito na za masafa marefu ambazo makundi halifu katika TPLF yalifaulu kuchukua awali. Hatua ya jeshi kukomboa magharibi mwa Tigray ni ushindi kwa wanajeshi wa Ethiopia waliokabiliana na mashambulizi na mauaji ya kikatili. Ni ushindi kwa raia wa Mai-Kadra waliokuwa wakiuawa kikatili na vikosi vya TPLF wiki hii.” Amesema Abiy.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy AhmedPicha: Minasse Wondimu Hailu/picture alliance/AA

Shirika linalowahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema kwamba machafuko yanayoendelea Ethiopia yamesababisha watu 14,500 kuyakimbia makwao kuingia Sudan, tangu mwanzo wa mwezi Novemba, huku idadi ya wahamiaji wapya ikizidi uwezo wa watoaji misaada.

Msemaji wa shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Geneva Babar Baloch, amesema miongoni mwa wahamiaji hao ni maelfu ya watoto ambao wamechoka na wamejawa hofu, na wengi walibeba tu akali ya vitu.

Mashahidi pia wameripoti kwamba baadhi ya waathiriwa walisema walitoka jimbo la Amhara ambalo limekuwa na historia ndefu ya mvutano na Watigray, hasa kuhusu umiliki wa ardhi.

Wahusika wa mauaji ya kikatili ni nani?

Shirika la Amnesty limesema halijaweza kuthibitisha upande upi umehusika katika mauaji hayo, lakini walioshuhudia wamesema kwamba vikosi vinavyounga mkono chama tawala katika jimbo hilo, Ukombozi kwa Watigray (TPLF) ndio walihusika.

Machafuko wa jimbo la Tigray yalianza mwanzo wa mwezi Novemba 2020Picha: Eduardo Soteras/AFP

Hata hivyo baadhi ya waathiriwa wanaokimbia machafuko na waliozungumza na shirika la habari la Reuters katika mji wa al-Fashqa nchini Sudan, wamedai kuwa walishambuliwa na vikosi vya serikali.

Serikali ya Ethiopia imesema walishambulia tu maeneo ya kijeshi ya vikosi vya Tigray ikiwemo maghala ya silaha na zana zao nyingine

Jeshi la Ethiopia pia limekanusha madai ya rais wa jimbo hilo kwamba limeshambulia bwawa la kuzalisha umeme katika jimbo la Tigray na hivyo kuacha wengi gizani.

Wakimbizi wa machafuko hayo ya Tigray wameelezea mashambulizi yaliyofanywa kwa ndege za kivita za serikali, watu kupigwa risasi mitaani na pia kukatwa kwa mapanga.

Ili kukabiliana na ongezeko la wahamiaji, Sudan imeidhinisha kambi kuwekwa Eneo la Um Rakuba kuwahifadhi wahamiaji 20,000.

(AFPE,APE, RTRE)

Mwandishi: John Juma

Mhariri: Gakuba, Daniel

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW