1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waonya kuwa hali Yemen ni ya lala salama

2 Juni 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameuambia mkutano wa wafadhili kuwa wafanyakazi wa huduma za kibinaadamu wamebakiwa na muda mchache kuweza kuzuwia janga kutokea nchini Yemen.

Antonio Guterres PK Covid-19
Picha: webtv.un.org

"Tupo kwenye muda wa lala salama. Kuishinda COVID-19 huku tayari nchi ikiwa kwenye hali mbaya ya kibinaadamu kunahitaji hatua za haraka," alisema katibu mkuu huyo ya Umoja wa Mataifa wakati akizungumza kwenye mkutano ulioitishwa kwa ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Saudi Arabia kwa njia ya mtandao hivi leo (Jumanne 2 Juni).

Saudi Arabia imeitisha mkutano huu ikidhamiria kukusanya dola bilioni 2.3 kuisaidia Yemen kukabiliana na mripuko wa virusi vya korona, yenyewe ikiwa mchangiaji mkubwa wa fedha lakini pia wa vita ambavyo vimeshapoteza maisha ya watu zaidi ya 100,000 na kuwasababishia wengine zaidi ya milioni 10 kuwa kwenye hatari ya kufa kwa njaa.

Kwenye taarifa yake, serikali ya Saudi Arabia imesema kwamba kiwango hicho cha fedha kinahitajika kwa ajili ya sekta mbalimbali za huduma za kibinaadamu, yakiwemo madawa, chakula na makaazi. 

Uingereza, ambayo inaongoza kwa kuiuzia silaha Yemen, imeahidi msaada mpya wenye thamani ya paundi milioni 160 kwa Yemen. Waziri wake wa Mambo ya Nje, Dominic Raab, amesema kwamba fedha hizo zitakuwa na maana kubwa kwa maisha ya maelfu ya Wayemeni, ambao mbali ya ufukara na vita, hivi sasa wanakabiliwa na janga la korona.

Waziri wa Misaada ya Kimaendeleo wa Uingereza, Anne-Marie Trevelyan, amesema fedha hizo zinalenga kuwahudumia watu 300,000 walio kwenye hali ngumu zaidi kila mwezi.

Yemen ni janga la kimataifa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihudhuria mkutano kuhusiana na vita dhidi ya COVID-19Picha: webtv.un.org

Upande wa Saudi Arabia kwenye mkutano uliwakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Faisal bin Farhan , huku kwa Umoja wa Mataifa, mbali ya Katibu Mkuu Antonio Guterres, naibu wake anayehusika na huduma za kiutu, Mark Lowcock, naye pia amehudhuria.

Lowcock ndiye ambaye amekuwa akipigania kwamba hadi kufikia mwishoni mwaka huu, Yemen iwe imeshapatiwa kitita cha dola bilioni 2.4, zikiwemo dola milioni 180 kupambana na janga la COVID-19.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa taifa hilo tayari linakumbwa na hali mbaya kabisa ya kibinaadamu kuwahi kushuhudiwa duniani.

Huku virusi vya korona vikisambaa, watu milioni 5.5 wako hatarini kutokuwa na uwezekano wa kupata maji wala chakula, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mashirika 24 ya misaada, likiwemo la Save the Children. 

Mashirika ya misaada yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kuendeshea miradi yao nchini Yemen, na hadi sasa asilimia 75 ya miradi hiyo imefungwa ama kusitishwa kwa muda.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW