1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waonya mgogoro wa kiutu huko Syria

Sylvia Mwehozi
14 Machi 2019

Wawakilishi wa ngazi za juu kutoka nchi zenye nguvu duniani na mashirika ya kimataifa, yanakutana katika juhudi za kupata misaada ili kuisaidia Syria.

Brüssel Syrien-Geberkonferenz
Picha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wataalamu wanaonya kuwa, mgogoro wa Syria ambao tayari umeua zaidi ya watu laki nne, na kusababisha ongezeko la wakimbizi kwa majirani wa nchi hiyo na ulaya, hauna dalili ya kwisha. Takribani asilimia 80 ya raia ambao bado wanaishi nchini humo wanaishi katika dimbwi la umasikini, huku wakimbizi wakisita kurejea nyumbani wakihofia machafuko na kuwekwa jela. Karibu raia milioni sita wameikimbia Syria, wengi wao wakiishi katika mazingira hatari nchini Uturuki na Jordan.

Akizungumzia hali ya Syria, mkuu wa masuala ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa Mark Lowcock amesema mgogoro wa Syria ni mbaya zaidi kuwahi kutokea. Lowckock pia ameeleza hofu yake  juu ya mgogoro unaoendelea kutokota wa Idlib iliyo Kaskazini mwa Syria ambapo zaidi ya watu 90 waliuawa mwezi uliopita, nusu yao wakiwa ni watoto.

Wajumbe wanaoshiriki mkutano wa kuichangia Syria mjini BrusselsPicha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Umoja wa Mataifa umesema, zinahitajika dola bilioni 3.3 kuisaidia Syria kwa mwaka huu pekee pamoja na bilioni zingine 5.5 zitakazosaidia nchi jirani ambapo raia wengi wa Syria hukimbilia. Takribani watu milioni 11.7 wanategemea misaada, na zaidi ya milioni 6 wamelazimika kuyakimbia makazi yao lakini wanaendelea kuishi nchini nchini humo.

Umoja wa Ulaya ambao ndio mfadhili mkubwa wa misaada duniani, ulitangaza kuwa utatoa Euro milioni 560 mwaka huu wakati wakipanga kutoa kiwango kama hicho mwaka ujao na mwaka 2021. Pia Mwakilishi mkuu wa sera za nje wa umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema kwamba kundi la mataifa 28 ya umoja huo, litaipatia Uturuki kiasi cha Euro bilioni 1.5 ili kuisaidia kumudu wakimbizi kutoka Syria ikiwa ni sehemu ya makubaliano na nchi hiyo kuzuia wakimbizi zaidi wasifike barani Ulaya.

Mogherini amesema Umoja wa Ulaya ambao ndio mwenyeji wa mkutano kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa wanatumaini kwamba mkutano huo wa wahisani utayapa msukumo mazungumzo ya amani chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa. '' Tunataka watu wa Syria wasisahaulike wakati ambapo jumuiya ya kimataifa''. Mogherini ameongeza kuwa,  ''hatuna budi  kuendelea kutafuta suluhisho la kudumu la kisiasa la mgogoro wa Syria.''

Katika mkutano huo wa Brussels, Syria haikuwa na mwakilishi. Si kutoka upande wa serikali wala wa upinzani kwani hawakuwa wamealikwa kuhudhuria. Hata hivyo wawakilishi wa asasi za kiraia mjini Brussels wanahofia kuwa nchi wahisani zinataka kuwashinikiza wakimbizi wa Syria kurejea makwao licha ya hatari wanazoweza kukumbana nazo.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Geir Pedersen akiwa na Mkuu wa Sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini Picha: picture-alliance/AA/D. Aydemir

Lakini pamoja na kutoa misaada, Umoja wa Ulaya umekataa kuijenga upya nchi hiyo hadi itakapokuwa na utulivu wa kisiasa. Hata hivyo baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali  yanaamini kwamba msimamo huo  unaweza kuwa kikwazo kikubwa katika juhudi za kutoa misaaada.

Mathew Hemsley, mshauri wa masiliano na sera wa shirika la OXFAM kwa upande wa Syria anasema Shirika

hilo halipo nchini humo kutengeneza mfumo mpya wa maji Syria wala kujenga mtandao mpya wa shule. Bali wako kwa ajili ya kuhakikisha watoto wanaweza kupatiwa elimu katika darasa ambalo mvua haiwezi kuingia kupitia madirisha yaliyovunjika na kwamba watu hawana maji machafu yanayotiririka kwenye nyumba zao.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW